Sunday, August 26, 2018

ACHIA SHOKA KAMATA MZINGA - RC SINGIDA, DKT. REHEMA NCHIMBI

MKUU wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi amekabidhi zawadi ya Mizinga ya Nyuki 12 kwa vijana sita (6) waliokimbiza Mwenge wa Uhuru 2018 mkoani Singida ambapo kila mmoja amepatiwa Mizinga miwili (2) ili kuunga mkono kampeni yake ya ACHIA SHOKA KAMATA MZINGA.

Dkt. Nchimbi amekabidhi Mizinga hiyo katika kikao cha Tathimini ya Mbio za Mwenge wa Uhuru 2018 uliokimbizwa mkoani Singida kuanzia tarehe 07/08/2018 hadi 14/08/2018, kikao kilichofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Singida vijijini.

Dkt. Nchimbi ametoa wito kwa kila mwananchi mkoani Singida kutunza manzingira na kuhakikisha kutokatwa miti kwaajili ya nishati ya mkaa badala yake kutundika mizinga ya Nyuki.

Katika hatua nyingine. Dkt. Nchimbi amewakabidhi Mizingi takribani 10 kwa wanafunzi zaidi ya 59 kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma na Sua waliokuja kuzungumza naye wakitokea Nyumba ya Nyuki ambapo walipokuwa wakifanya mafunzo ya wiki 5 (Field) ambapo mizingia hiyo ilikabidhiwa kwa wanakikundi cha NAHARI GROUP kilichopo kata ya Mtamaa halmashauri ya Manispaa ya Singida.


Mkuu wa mkoa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akiwa katika picha ya pamoja na Wanafunzi zaidi ya 59 kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma na Sua, pamoja na maofisa wa Halmashauri na Sekretarieti ya Singida.

WAKATI WA MBIO ZA MWENGE WA UHURU 2018
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru 2018 Kitaifa Bw. Charles Kabeho kila alipokuwa akizungumza na wananchi wa mkoa wa Singida wakati wa kutoa salamu na ujumbe wa Mwenge wa Uhuru 2018, aliwataka wazazi na walezi kutafsiri vyema maelekezo ya Serikali.

Kabeho alisema kuwa, wazazi na walezi ni vyema kuunga mkono dhana ya Serikali iliyotolewa kuhusu elimu bila malipo kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha nne ili kuondoa kero na kuendelea kuendelea kuboresha sekta hiyo. Kabeho alifafanua kuwa, Serikali imetoa maelekezo hayo na kufuta michango iliyokuwa inadaiwa shule za msingi na sekondari iliyosababisha kero kubwa kwa wanafunzi na wazazi.

Alisema pamoja na agizo hilo la Serikali bado wazazi na walezi na jamii kwa ujumla wanahitajika katika kuchangia vifaa vya watoto wao, ujenzi wa miundombinu ya madarasa, nyumba za walimu, maabara na chakula cha mchana kadiri inavyowezekana.
Michango hiyo lazima ifuate makubaliano ya kamati ya shule za msingi, kamati za maendeleo za mitaa, vijiji na bodi za shule za sekondari kwa kuweka utaratibu mzuri wa ukusanyaji na kudhibiti matumizi yake alisema Kabeho.

Alibaini kuwa mbali na hali hiyo Serikali inaendelea kuchangia kuinua hali ya taaluma, kwa kusaidia ukamilishaji wa madarasa, nyumba za walimu, vifaa vya maabara, kupeleka walimu, kuongeza nafasi za kidato cha sita sambamba na idadi ya wanafunzi wa vyuo vikuu na vyuo vya ufundi nchini.

Mwenge wa Uhuru 2018, katika Mkoa wa Singida umekimbizwa kwa muda wa siku (7), katika Halmashauri saba (7) kwa kuanzia na Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni tarehe 07/08/2018 na kuhitimisha mbio zake mkoani Singida mnamo tarehe 13/08/2018 ambapo tarehe 14/08/2018 ukakabidhiwa mkoani Simiyu.

Aidha, Wananchi wa Mkoa wa Singida wameupoke vema ujumbe wa Mwenge wa Uhutu mwaka 2018 ambao umetolewa maeneo mbalimbali ya Wilaya za Mkoa wa Singida ambao ni ELIMU NI UFUNGUO WA MAISHA; WEKEZA SASA KWA MAENDELEO YA TAIFA LETU.

Kwaupande wake, Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi amewapongeza ndugu wakimbiza Mwenge wa Uhuru 2018 wakiongozwa na Ndugu Charles Kabeho kwa kuleta ujumbe Mkuu na Ujumbe Mwambatano wa Mwenge wa Uhuru 2018 kwa umahiri mkubwa sana.

Ninyi ni walimu sahihi kwa darasa la Mkoa wa Singida, Mmetufundisha pia kuhusu: Mapambano dhidi ya Rushwa, chini ya kaulimbiu; KATAA RUSHWA JENGA TANZANIA.
Mapambano dhidi ya Dawa za kulevya, chini ya kaulimbiu; TUWASIKILIZE NA KUWASHAURI WATOTO ILI WASITUMIE DAA ZA KULEVYA.
Mapambano dhidi ya Malaria, chini ya kaulimbiu; SHIRIKI KUTOKOMEZA MALARIA KWA MANUFAA YA JAMII.

Mapambano dhidi ya UKIMWI chini ya kaulimbiu; MWANANCHI JITAMBUE: PIMA AFYA YAKO SASAAlisema Dkt. Rehema Nchimbi.

Dkt. Nchimbi alisema kuwa Serikali ya Mkoa kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali inaendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya madhara ya Rushwa, Dawa za kulevya, UKIMWI na VVU na Malaria. Elimu hii inatolewa kupitia njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na Vyombo vya Habari, Machapisho, Mabango na Vikundi mbalimbali vinavyotoa ushauri wa namna ya kujikinga na tabia hatarishi ili kuufanya Mkoa wa Singida kuwa salama.

"USIKATE MSITU, FUGA NYUKI KISASA KWA MBINU BORA UJIKWAMUE KIUCHUMI" Dkt. Rehema Nchimbi.

No comments:

Post a Comment