Kaimu Katibu Tawala
Sehemu ya Maji Mkoa wa Singida Mhandisi Lyidia Joseph akizungumza na timu ya
usimamizi wa sekta ya maji ya halmashauri ya Manyoni, wa kwanza kulia kwake ni Diwani
wa Kata ya Mkwese na Mwenyekiti wa huduma za Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya
Manyoni Robert Kenze.
Mhandisi wa Maji wa
Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Gasto Mbondo pamoja na wajumbe wengine wa timu
ya usimamizi wa sekta ya maji hiyo wakimsikiliza kwa makini Kaimu Katibu Tawala
Sehemu ya Maji Mkoa wa Singida Mhandisi Lyidia Joseph (hayupo pichani).
Mhandisi wa Maji
kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Athanas Nziku akichangia hoja katika kikao kati ya
wataalamu wa sekta ya maji Mkoa na timu ya usimamizi wa sekta ya maji ya
halmashauri ya Manyoni.
Baadhi ya wahandisi
wa maji Mkoa wa Singida wakifuatilia kwa umakini kikao cha ufuatiliaji wa
utekelezaji wa miradi ya maji kati yao na timu ya usimamizi wa sekta ya maji wa
Halmashauri ya wilaya ya Manyoni.
Ofisi ya Mkuu wa Mkuu
wa Mkoa wa Singida imedhamiria kusimamia uboreshaji wa huduma za maji mkoani
hapa huku mizaha itakayofanywa na mtu yeyote katika miradi ya maji,
kutovumiliwa.
Kaimu Katibu Tawala
Sehemu ya Maji Mkoa wa Singida Mhandisi Lyidia Joseph amebainisha hayo leo
wakati wa kikao maalumu na Timu ya usimamizi wa sekta ya maji ya halmashauri ya
Wilaya ya Manyoni, kwa ajili ya
kufuatilia usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maji.
Mhandisi Lydia
amewaeleza wataalamu hao kuwa uongozi wa mkoa hautavumilia endapo kuna mtumishi
yeyote atafanya mzaha katika kusimamia miradi ya maji kwakuwa mkoa umekuwa
ukitoa ushirikiano wa kutosha hivyo hakuna sababu ya kushindwa kufanya vizuri.
“Sisi katika ngazi ya
mkoa hatutavumilia mzaha katika masuala ya maji, tupo tayari kutoa ushirikiano
popote mnapoona mnakwama ili tu tufikie malengo yetu ya kutoa huduma bora za
maji kwa wananchi, hali ilivyo sasa hairidhishi kabisa, tufanye kazi kwa kasi
zaidi”, ameongeza Mhandisi Lydia.
Amesema, halmashauri
hiyo inapaswa kuhakikisha inatekeleza agizo la Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt
Rehema Nchimbi la kuongeza asilimia ya upatikanaji wa maji katika halmashauri
hiyo kutoka 45 hadi 72 ifikapo mwezi Juni, 2018 pamoja na kuandaa takwimu
sahihi za upatikanaji wa maji ifikapo Disemba mwaka huu.
Mhandisi Lydia
amefafanua kuwa halmashauri hiyo itaweza kuongeza asilimia ya upatikanaji maji na
kufikia lengo la asilimia 72 endapo watendaji wote hasa wajumbe wa timu ya
usimamizi wa sekkta ya maji, watashirikiana kusimamia ujenzi wa miradi mitano pamoja
na ukarabati wa miradi minne iliyopo kwenye bajeti.
“Kila Mjumbe hapa ana
kazi ya kufanya katika miradi hii ya Makanda, Nyaranga, Kikombo, Makutopola na
Kicheho inayojengwa pamoja na ile ya Sanza, Mkwese, Londoni na Sorya inayokarabatiwa,
Kitengo cha ugavi kisimamie taratibu za manunuzi zinafuatwa pamoja na kuhakiki
ubora wa mkandarasi, mwanasheria aelekeze taratibu za kisheria, Maendeleo ya
jamii ahakikishe wananchi wanaujua mradi vizuri, kila mmoja akitekeleza jukumu
lake ipasavyo tutafikia lengo”, ameeleza na kuongeza kuwa,
“Idara ya maji
msifanye siri miradi ya maji na kujifungia wenyewe hakikisheni timu hii ya
usimamizi wa sekta yenu inafahamu vizuri miradi yote ya maji pamoja na
kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo, mkifanya hivyo mtaenda kwa kasi na kazi
itafanyika kwa ufanisi, sio kila kitu mfanye wenyewe tu”, ameongeza Mhandisi
Lydia.
Aidha Mhandisi Lydia
amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Charles Fussi kwa
kujitoa kwake katika kusimamia na kutoa fedha za kusaidia miradi ya maji akitoa
mfano wa kiasi cha milioni 16 zilizotolewa na mkurugenzi huyo kutoka katika
makusanyo ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji.
Naye Mhandisi wa Maji
kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Athanas Nziku ameieleza timu hiyo kuwa usimamizi
wa jumuiya za watumia maji ni jambo muhimu kwakuwa takwimu zimeonyesha jumuiya
hizo zimekuwa zikikusanya pesa nyingi sambamba na matumizi makubwa ya fedha
wanazokusanya.
Mhandisi Nziku
amewafafanulia kuwa jumuiya hizo za watumia maji zinapokusanya fedha nyingi
sambamba na kutumia fedha nyingi ni moja ya kiashiria kuwa miradi hiyo ya maji
inaweza kufa hivyo wazitembelee na kuona tatizo liko wapi endapo liko ndani ya
uwezo wa halmashauri liweze kutatuliwa mapema.
Kwa upande wake
Diwani wa Kata ya Mkwese na Mwenyekiti wa huduma za Jamii wa Halmashauri ya
Wilaya ya Manyoni Robert Kenze amesema, halmashauri hiyo imedhamiria kuboresha
huduma za maji ambapo ajenda ya maji imewekwa kipaumbele katika vikao vyote
muhimu.
Kenze amesema wakuu
wa Idara wa halmashauri hiyo watashirikiana na Idara ya maji wilayani humo huku
wanasiasa wakiwa tayari kutoa elimu na kusimamia utekelezaji wa miradi ya maji.
No comments:
Post a Comment