Meneja Msimamizi
Maarifa na Mawasiliano kutoka shirika la AMDT Al-amani Mutarubukwa (aliyevaa
miwani) akiwaonyesha wakulima na wasindikaji mbegu za alizeti za Chotara kabla
ya kufanya majaribio ya usindikaji yaliyoonyesha kuwa mbegu za chotara zinatoa
mafuta na mashudu mengi kuliko mbegu za zamani.
Mwakilishi wa Meneja
wa Faida Mali Mary Daniel akiwaonyesha wakulima na wasindikaji tofauti kati ya mbegu
za alizeti za Chotara na zile za zamani kabla ya kufanya majaribio ya
usindikaji yaliyoonyesha kuwa mbegu za chotara zinatoa mafuta na mashudu mengi
kuliko mbegu za zamani.
Wakulima na wasindikaji wakishiriki usindikaji wa mbegu za alizeti chotara na zile za zamani katika majaribio yaliyoonyesha kuwa mbegu za chotara zinatoa mafuta na mashudu mengi kuliko mbegu za zamani.
Afisa Kilimo Kutoka
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Mashaka Mlangi akikagua mashudu wakati wa
majaribio ya usindikaji wa mbegu za alizeti ambapo matokeo yameonyesha kuwa
mbegu chotara zinatoa mafuta na mashudu mengi kuliko zile za zamani.
Mkulima aliyeshiriki
majaribio ya kulima mbegu chotara za alizeti Kutoka Ihanja Wilayani Singida John
Thomasi akitoa ushuhuda wa ubora wa mbegu hizo kwa wakulima wengine wa alizeti
(hawapo pichani).
Wakulima na
wasindikaji wa zao la Alizeti Mkoani Singida wameonekana kufurahia na kupata
matumaini mapya mara baada ya kushuhudia matokea ya majaribio ya usindikaji wa
mbegu chotara ya Alizeti mkoani Singida.
Wakulima na wasindikaji
hao wameshuhudia majaribio ya usindikaji wa mbegu chotara ya alizeti yakifanyika
katika kiwanda cha kukamua mafuta ya Alizeti cha Nuru mjini Singida, kwa
kukamua mbegu chotara na zile za zamani kisha kulinganisha kiwango cha mafuta
na mashudu yaliyopatikana.
Mbegu chotara
zilizofanyiwa majaribio zimepandwa na wakulima mkoani hapa ikiwa ni sehemu ya
majaribio hayo, ambapo matokeo yameonyesha kuwa mbegu chotara zinatoa mazao
mengi, mafuta na mashudu mengi, zinatumia muda kidogo shambani mpaka kuvunwa, zinatumia
maji kidogo na hazishambuliwi na magonjwa ikilinganishwa na mbegu za zamani.
Mmoja kati ya
wakulima aliyeshiriki majaribio ya kulima mbegu hizo Kutoka Ihanja Wilayani
Singida John Thomasi alihudhuria pia majaribio ya usindikaji wa mbegu hizo na
kusema kuwa sasa wakulima wa alizeti wamepata mwanga kwa kuona namna ambavyo kilimo
cha alizeti kwa kutumia mbegu chotara ya alizeti kitawakomboa.
“Mimi ni mmoja kati
ya waliolima hizo mbegu chotara kama sehemu ya majaribio na tuliona kwa kuanzia
shambani hazisumbui, zinatumia maji kidogo, na mavuno ni mengi, kilichobaki
ilikuwa ni kujua ubora wake katika kutoa mafuta na mashudu jambo ambalo
tumeshuhudia leo kuwa mbegu hizi zinatoa mafuta mengi kuliko zile za zamani”,
amesema Thomasi
Meneja Msimamizi
Maarifa na Mawasiliano kutoka shirika la AMDT Al-amani Mutarubukwa amesema
shirika hilo linalojikita katika Kilimo cha alizeti nchini hasa katika kuboresha
mfumo wa masoko, uzalishaji na usindikaji lilifanya utafiti ulioonyesha kuwa
changamoto kubwa ya wakulima wa alizeti ni kutokuwa na mbegu bora.
Mutaburukwa amesema kwakuwa
mbegu zilizokuepo zimekuwa hazitoi mazao ya kutosha Shirika hilo lilifadhili
majaribio ya mbegu chotara Mkoani Singida kupitia mradi wa Faida Market link
kwa kuwezesha wakulima kupanda mbegu hizo.
Ameongeza kuwa matokeo
ya majaribio hayo yamekuwa mazuri ambapo kwa upande wa mavuno mbegu chotara
zimethibitika kutoa mazao mengi ambapo kwa ekari moja mkulima mmoja ameweza
kuvuna gunia 16 ambapo kwa mbegu za zamani angeweza kuvuna gunia 3 mpaka tano.
Mutaburukwa amesema “Mara
baada ya kuvunwa kwa alizeti hiyo AMDT pia imefanya majaribio ya kusindika mbegu
hizo ambapo kilogram ishirini za mbegu chotara zimetoa mafuta lita sita ambapo
mbegu za zamani zimetoa lita tano kwa kilo hizo hizo, huku mashudu yakipatikana
kilogram 14 kwa mbegu chotara tofauti na kilogram 13 za mbegu za zamani.
Ameongeza kuwa Sifa
ya mbegu hizo chotara ni kutoa mazao mengi, kutumia maji kwa ufanisi, zinastawi
katika udongo wa aina zote, na pia hazikai shambani mda mrefu kabla ya kuvunwa ambapo
hutumia siku 84 mpaka kuvuna tofauti na siku 97 kwa mbegu za zamani.
Naye Mwakilishi wa Meneja
wa Faida Mali Mary Daniel amesema majaribio ya mbegu chotara yalianza mwenzi wa
nne na yalihusisha halmashauri nne ambazo ni Mkalama, iramba, ikungi na
Singida, ambapo mbegu ziliyotumika katika kufanya majaribio ya usindikaji zililimwa
Kijiji cha ihanja wilaya ya ikungi.
Mary amesema wakulima
waliofika kushuhudia majaribio ni 25 na wasindikaji 12 kutoka katika wilaya ya
singida na ikungi ambao kwa pamoja wameazimia kutumia mbegu ya chotara na
kuwaelimisha wakulima wenzao faida ya mbegu hizo.
Ameongeza kuwa
makampuni mawili ya SDC na BYTRADE wamejiandaa kusambaza mbegu chotara kwa
wakulima wa mkoa wa Singida huku akiwahakikishia wakulima kuwa wasambazaji hao
wataleta mbegu kwa wakati ili wapande ndani ya msimu wa kilimo.
No comments:
Post a Comment