Sunday, November 26, 2017

MICHAKATO IMECHELEWESHA UPATIKANAJI WA MAJI IRAMBA.



hKatibu Tawala Msaidizi Huduma za Maji Mhandisi Lydia Joseph akiandika maoni ya wajumbe wa kikao cha ufuatiliaji wa miradi ya maji katika halmashauri ya Iramba, Kusoto kwake ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Iramba Simioni Tiyosera.
Baadhi ya wakuu wa idara na vitengo wakifuatilia kikao cha ufuatiliaji wa miradi ya maji katika halmashauri ya Iramba.

Mlolongo wa michakato na taratibu ambazo zimekuwa zikitekelezwa kwa kasi ndogo imekuwa sababu ya kuchelewesha kukamilika kwa miradi ya maji hivyo kusababisha ukosefu maji safi na salama Wilayani Iramba.

Katibu Tawala Msaidizi Huduma za Maji Mhandisi Lydia Joseph ameeleza hayo wakati wa kikao cha ufuatiliaji wa miradi ya maji katika halmashauri hiyo ambapo ameeleza kuwa kasi ya utekelezaji wa miradi ya maji katika halmashauri hiyo ni ndogo.

Mhandisi Lydia ameeleza kuwa licha ya kufikia kipindi cha nusu ya mwaka wa fedha, halmashauri hiyo imetekeleza miradi ya maji kwa asilimia moja tu, huku maelezo ya kwanini hawajafikia asilimia 50 inayotakiwa yakiwa ni kuwa wanaendelea na michakato.

“Tupo nusu ya mwaka wa fedha na miradi imetekelezwa kwa asilimia moja, maelezo ya kuwa mpo katika michakato kwakweli hayaridhishi, mwananchi hataki kusikia michakato, anataka maji”, ameeleza Mhandisi Lydia na kuongeza kuwa,

“Michakato na taratibu hizo mnazifanya kwa kasi ndogo sana, michakato mingine inahusisha vikao ambapo unakuta mnachelewesha kwa kigezo cha kusubiri mpaka fedha zipatikane, kwakweli mmechelewa sana, naomba tuwe wabunifu hasa katika sekta hii muhimu kwa maendeleo ya taifa letu”, amefafanua.

Aidha amewaeleza kuwa ili kuharakisha upatikanaji wa maji, miradi yote ya uchimbaji wa visima ikianza, usanifu wa mtandao wa usambazaji wa maji nao uanze mara moja ili kisima kikikamilika na usambazaji wa maji ufanyike haraka.

“Hata Mkichimba visima vingi bila ya kuharakisha usambazaji wa maji kwa wananchi bado mtakuwa hamjamsaidia huyu mwananchi anayekosa maji, nawashauri kasi ya kuchimba visima iendane na kasi a kuyasambaza maji kwa wananchi”, amesisitiza Mhandisi Lydia.

Aidha amewasisitiza kuweka mikakati inayotekelezeka na sio kutoa majibu mazuri kwa timu inayofanya ufuatiliaji wa miradi ya maji kwa lengo la kumaliza vikao, bali mikakati wanayoweka iwe ile inayotekelezeka na kuleta ufanisi katika kupandisha upatikanaji maji kutoka asilimia 47.5 ya sasa mpaka lengo la mkoa la asilimia 72.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmshauri ya Iramba Linno Pius Mwageni ameeleza kuwa, kuchelewa kwa miradi ya maji kumesababishwa na baadhi ya wakandarasi ambao wamekuwa wakisua sua kutekeleza miradi waliyopewa, ijapokuwa kwa sasa wamepewa onyo kali hivyo wanatekeleza kazi zao kwa kasi.

Mwageni amefafanua kuwa kwa sasa ana imani kuwa miradi ya maji itakamilika kwa muda kwakuwa fedha zipo za miradi hiyo na pia halmashauri itaimarisha ufuatiliaji ili ikamilike katika ubora unaotakiwa.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Iramba Simioni Tiyosera amemuomba Mhandisi wa Maji wa Mkoa kuimarisha usimamizi wa wahandisi wa maji wa ngazi ya halmashauri ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi pamoja na kuwasiadia kwa ushauri pale wanapokwama.

No comments:

Post a Comment