Monday, August 28, 2017

WANAWAKE WA SINGIDA WAHIMIZWA KUACHA WOGA, WAPIGANIE HAKI ZAO.



Mratibu wa shirika la Singida IR Vicoba Net work (SIRVICONET) Happy Francis, akitoa ufafanuzi wa jambo kuhusu mafunzo juu ya umiliki ardhi kwa wanawake. Mafunzo hayo yamefanyikia kwenye ukumbi wa mikutano kituo cha walimu barabara ya Nyerere mjini hapa.



Baadhi ya washiriki wa mafunzo juu ya umiliki wa ardhi kwa wanawake yaliyoandaliwa na shirika la SIRVICINET na kufadhiliwa na shirika la The Foudation For Civil Society.


Wanawake Mkaoni Singida wamehimizwa kujenga utamaduni wa kujiamini na kuondoa woga, ili waweze kufanikiwa kupigania haki zao za msingi, ikiwemo ya haki ya kumiliki ardhi.

Wito huo umetolewa na diwani wa kata ya Mungumaji Hassan Shabani Mkata, wakati akichangia mada juu ya haki ya umiliki wa ardhi kwa wanawake kwenye mafunzo yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kituo cha walimu mjini hapa.

Mafunzo juu ya haki ya mwanamke kumiliki ardhi yaliandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Singida IR Vicoba Net Work (SIRVICONET) na kufadhiliwa na shirika la The Foundation for Civil Society kwa ajili ya wanawake wa Singida.

Mkata amefafanua kuwa katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua uhalali wa umiliki ardhi kwa wanawake, isipokua wanawake wenyewe wanakosa haki hiyo kutokana na woga wao uliopitiliza.

Amesema umefika wakati sasa wanawake wawe mstari wa mbele kupingania haki zao na kutokomeza mila kandamizi, ziliyopitwa na wakati ambazo zinawakandamiza kwamba hawana haki ya kumiliki ardhi.

“Kwa hilo wanawake watafanikiwa tu endapo wataondoa woga, wakajiamini na wakaunganisha nguvu zao. Nasisitiza, wanawake wanapaswa kutambua kuwa wanahaki sawa na wanaume, katika kumiliki ardhi”, amefafanua.

Naye mwezeshaji wa mafunzo hayo Afisa Ardhi kutoka Manispaa ya Singida, Lilian Msasi amesema ardhi ni mali ya umma na imekabidhiwa kwa rais, kwa niaba ya Watanzania wote.

“Raia wote…. wanawake na wanaume wana haki sawa ya kupata, kumiliki, kutumia na kugawana ardhi. Miliki za ardhi zilizopo zinatambuliwa na kulindwa kisheria”, amesema Msasi.

Msasi amesema mwanamke ana haki sawa na mwanaume katika kupata, kumiliki, kutumia na kugawa ardhi. Haki hiyo imetamkwa kwenye kifungu cha tatu (92) cha sheria ya ardhi mjini na sheria ya vijiji za mwaka 1999.

Kuhusu sifa za kuomba haki ya kumiliki ardhi, Lilian amesema kuwa ni mtu ye yote mwanamke au mwanaume, mtanzania mwenye umri wa miaka 18 na kuendelea anaweza kupatiwa hati ya kumiliki ardhi.

“Pia kikundi cha watu ambao sio raia wa Tanzania, wanaweza kuomba haki ya kumiliki ardhi (delivative righs), kwa ajili ya uwekezaji”, amesema.
Ameongeza kuwa kwa vile wanawake ni watumiaji wakuu wa ardhi, vyombo vinavyohusika na masuala ya usimamizi na utendaji wa ardhi, vihakikishwe kuwa wanawake na wanaume wanashirikishwa ipasavyo katika masuala yahusuyo ardhi

Awali Mratibu wa Shirika la SIRVICONET, Happy Francis, amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo zaidi wajumbe wa mabaraza ya ardhi ya kata, maafisa watendaji wa kata na maafisa maendeleo ya jamii, ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Ameongeza kuwa dhamira ya SIRVICONET ni kuwezesha wanachama wake kuwa na nguvu kiuchumi katika kupambana na umaskini, ujinga na maradhi na kuwa na mahusiano mazuri miongoni mwao.

Mwezeshaji Lilian Msasi, akitoa mafunzo juu ya umiliki wa ardhi kwa wanawake yaliyoandaliwa na shirika la SIRVICONET na kufadhiliwa na shirika la The Foundation For Civil Society.

No comments:

Post a Comment