Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mheshimiwa Suleiman Jafo
akimkabidhi mshindi wa tatu wa maonyesho ya nanenane kanda ya kati ambaye ni Jeshi
la Magereza.
Naibu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)
Mheshimiwa Suleiman Jafo amezitaka halmashauri zote nchini kutekeleza jukumu
lao la kuwapelekea wakulima wa vijijini teknolojia na pembejeo bora ili
kuongeza tija katika shughuli za uzalishaji mali.
Jafo
ametoa rai hiyo jana wakati wa kilele cha maonyesho ya nanenane kanda ya kati
inayojumuisha mikoa ya Singida na Dodoma ambapo alipata fursa ya kutembelea
mabanda mbalimbali yalioonyesha shughuli za kilimo na ufugaji pamoja na sekta
binafsi zinazosaidia katika kukuza uchumi.
Amesema
kauli mbiu ya maonyesho hayo kwa mwaka huu ni “Zalisha kwa Tija Mazao na Bidhaa za Kilimo,
Mifugo na Uvuvi ili kufikia Uchumi wa Kati” hivyo basi halmashauri
zinatakiwa kuhakikisha mazao ya wakulima na wafugaji yanapata soko kwa kutoa
elimu ya kuchakata na kufungasha bidhaa zao katika ubora unaokubalika sokoni
ili mazao hayo yawe na thamani zaidi.
Jafo
amesema halmashauri zote zinapaswa kutekeleza wajibu wao kwa kutenga maeneo kwa
ajili ya uwekezaji wa viwanda na kuhakikisha maeneo hayo yanakuwa na huduma
zote za msingi kama vile miundombinu ya Barabara, Umeme na Maji ili kuwavutia
wawekezaji na hivyo kumsaidia mkulima na mfugaji kufikia uchumi wa kati.
Kwa
upande wake Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa William Ole
Nasha ameipongeza Benki ya Maendeleo ya Kilimo kwa kuendelea kuwezesha shughuli
za kilimo nchini huku akitoa angalizo la kutowasahau wakulima wasio na uwezo.
Ole
Nasha amesema Benki hiyo isitoe mikopo kwa wakulima wakubwa na wenye uwezo tu
bali isisahau jukumu la kuwafikia wakulima wasio na uwezo ili waweze kupata
mikopo na kuweza kulima kisasa kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.
Wakati
huo huo Naibu waziri Jafo ametoa Wito kwa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi
kuamua kuufanya Mkoa wa Dodoma hasa Viwanja vya Nzuguni kuwa Kituo cha Kudumu
cha Maonesho ya nanenane kitaifa kutokana na Kijiografia kuwa katikati na Makao Makuu ya
nchi na hivyo kuwa rahisi kwa Kanda zote nchini na hata nchi za jirani kuja
kushiriki Maonesho ya Nane Nane.
Jafo
amesema hayo akiunga mkono kauli iliyotolewa na Waziri wa Kilimo Mifugo na
Uvuvi Mheshimiwa Dkt. Charles Tizeba aliyesema Serikali inafikiria kuachana na
utaratibu wa kuhamisha hamisha Maonesho
ya kitaifa ya Nane Nane kwenye Kanda mbalimbali na badala yake kuwa na kituo
kimoja cha Kitaifa kama ilivyo kwa maonesho ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba)
yanavyofanyika Dar es Salaam pekee.
Jafo
amesema Uwanja wa Nane Nane Nzuguni unahitaji kufanyiwa uwekezaji na
uendelezaji wa miundombinu yake kama barabara, umeme na maji na kuboreshwa
huduma mbalimbali na kuzitaka Mamlaka za Serikali za Mikoa ya Dodoma na Singida
kuweka mkakati wa kuendeleza miundombinu hiyo kwa kuwa baada ya uwekezaji
mkubwa uwanja huo utarejesha mapato mengi.
Ameongeza
kuwa Serikali za Mikoa ya Singida na Dodoma inaweza kufanikisha ukarabati huo
kwa kushirikisha wadau mbalimbali wakiwemo Taasisi kama Benki ya Uwekezaji TIB
na Benki ya Maendeleo ya Kilimo TADB.
Washindi
wa Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Kati yaliyoanza tangu Agosti Mosi ni Jeshi la
Kujenga Taifa (JKT) lililoibuka kuwa Mshindi wa jumla wa Maonesho ya Mwaka huu,
likifuatiwa na Benki Kuu ya Tanzania ikiwa mshindi wa pili na Mshindi wa tatu akiwa
ni Jeshi la Magereza.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mheshimiwa Suleiman Jafo
akimkabidhi mshindi wa tatu wa maonyesho ya nanenane kanda ya kati ambaye ni Jeshi
la Magereza.
No comments:
Post a Comment