Mkuu wa Mkoa wa
Tabora Aggrey Mwanry ambaye alikuwa ni Mwenyekiti wa mkutano wa ujirani mwema
wa Mikoa 11 akitoa tamko la kumpongeza Rais Magufuli, kulia kwake ni Mwenyeji
wa Mkutano huo Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi.
Wajumbe wa kamati
za Ulinzi na Usalama za mikoa 11 iliyoshiriki Mkutano wa Ujirani mwema
wakifurahia mada zilizowasilishwa katika Mkutano huo uliofanyika katika ukumbi
wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida.
Mkuu wa Mkoa wa
Tabora Aggrey Mwanry (katikati) ambaye alikuwa ni Mwenyekiti wa mkutano wa
ujirani mwema wa Mikoa 11 akipokea maoni na mawazo ya wajumbe wa kutano huo,
kulia kwake ni Mwenyeji wa Mkutano huo Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema
Nchimbi.
Wakuu wa Mikoa 11 wametoa tamko la
kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kutokana
na kazi ya kizalendo ya kutetea na kulinda rasilimali za Watanzania kwa maslahi
ya taifa zima.
Tamko hilo limetolewa jana jioni
wakati wakuu hao wakihitimisha mkutano wa kawaida wa ujirani mwema baina ya mikoa
hiyo ambao umefanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa
Singida.
Wakiongozwa na Mwenyekiti wa
mkutano huo ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanry wakuu wa mikoa ya Singida,
Rukwa, Katavi, Kagera, Dodoma, Manyara, Geita, Shinyanga, Mwanza na Kigoma
wamesema wanamuunga mkono Rais na wataendelea kuzingatia maelekezo yake katika
utendaji wao.
“Sisi wasaidizi wake (rais
Magufuli) tutaendelea kutekeleza na kuzingatia maelekezo katika
utendaji wetu wa kila siku. Aidha, wakati wote tutakuwa pamoja na wananchi na
kuwatumikia kwa kutimiza wajibu wetu kwa uaminifu, uadilifu na tutahakikisha
maslahi ya wananchi na taifa yanapewa kipaumbele cha kwanza”, sehemu ya nukuu
ya tamko hilo.
Katika tamko hilo pia wametoa wito
kwa wananchi na wawekezaji wote halali wa ndani na nje ya nchi kumuunga mkono
rais Magufuli kwa kazi nzuri ya kulinda rasilimali za taifa na wakati wote wazingatie
sheria za nchi.
“Tutumie fursa nyingi zinazoendelea
kutengenezwa kwa hatua hizo za kizalendo anazochukua mheshimiwa mpendwa wetu
rais Dkt. Magufuli Kwa mafanikio, maendeleo na tija kuelekea Tanzania ya uchumi
wa kati na uchumi wa viwanda”, sehemu nyingine ya tamko hilo.
Katika Mkutano huo Mwenyekiti Mwanry
amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Singida kwa kuandaa mkutano huo na kupendekeza
mikutano ya ujirani mwema ya mikoa ifanyike kikanda ili kuimarisha ulinzi na
usalama wa taifa pamoja na kubadilishana uzoefu na kupeana taarifa mbalimbali
za kimaendeleo.
“Tumekutana hapa kwa mapenzi ya
nchi yetu na ya rais wetu Magufuli. Tuliokutana leo hii changamoto za mikoa
yetu zinafanana. Changamoto hizi ni pamoja na uharibifu wa mazingira, uhaba wa
mvua, kilimo cha kuhama hama na uhamiaji haramu”, amesema Mwanry na kuongeza;
“Kwa hiyo tukiacha kila Mkoa utatue
changamoto hizi kivyake hatutafanikiwa kizitatua. Tumekubaliana kukutana mara
kwa mara ili changamoto zinazotukabili sote tuzipatie ufumbuzi wa kudumu kwa
pamoja”.
Aidha, mwenyekiti huyo amesema
wamekubaliana kusimamia matumizi bora ya ardhi pia kusimamia ulinzi na usalama
hasa kwa Mikoa ile iliyopo mipakani na nchi jirani.
Kwa upande wake Mwenyeji wa Mkutano huo Dkt Rehema Nchimbi amesema
mkutano huo umekua wa manufaa makubwa kwa mikoa iliyohudhuria pamoja taifa kwakuwa
wameweza kubadilishana mawazo kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wote.
Wajumbe wa kamati
za Ulinzi na Usalama za mikoa 11 iliyoshiriki Mkutano wa Ujirani mwema
wakifuatilia mada zikiwasilishwa katika Mkutano huo uliofanyika katika ukumbi
wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida.
Mwenyeji wa
Mkutano wa ujirani mwema baina ya mikoa 11, Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema
Nchimbi akizungumza na wajumbe wa mkutano huo.
No comments:
Post a Comment