Katibu Mkuu Ofisi ya
Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma Dkt. Laurean Ndumbaro (katikati) akizungumza
na watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida (hawapo pichani) kama sehemu
ya maadhimisho ya wiki ya utumishi wa Umma kulia kwake ni Katibu Tawala Mkoa wa
Singida Dkt. Angelina Mageni Lutambi na Kushoto kwake ni Afisa Utumishi kutoka
Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Nsajigwa.
Katibu Mkuu Ofisi ya
Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma Dkt. Laurean Ndumbaro akizungumza na watumishi
wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida (hawapo pichani) kama sehemu ya maadhimisho
ya wiki ya utumishi wa Umma.
Watumishi wa Ofisi ya
Mkuu wa Mkoa wa Singida wakimsikiliza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi
wa Umma Dkt. Laurean Ndumbaro alipowatembelea katika kuadhimisha wiki ya
utumishi umma.
Katibu Mkuu Ofisi ya
Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma Dkt. Laurean Ndumbaro amewataka viongozi na
watumishi wote nchini kuzingatia nidhamu kama msingi wao wa utendaji kazi pamoja
na kanuni na maadili ya utumishi wa umma ili utumishi wao uweze kuwa mzuri.
Dkt. Ndumbaro
ameyasema hayo alipokutana na watumishi Mkoani Singida na kusikiliza matatizo, kero,
changamoto pamoja na kupata maoni ya namna ya kuboresha utumishi wa umma kama
sehemu ya maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma nchini.
Amesema kila mtumishi
anapaswa kufanya kazi kwa bidii na kwa nidhamu ya hali huku akiwasisitiza
viongozi hasa wa watumishi wa umma kuwasikiliza watumishi wao pale wanapotoa
maoni yao bila kuyapuuzia au kuwakatisha tamaa kwa vitisho.
“Ukiwa kiongozi
unapaswa uweze kuishi na kila aina ya mtu, kuna watumishi wengine hawawezi
kufichaficha mambo ukikosea wanakusema bila kupepesa maneno, wengine ni waoga
hawawezi kukueleza wazi ila wanatumia mbinu mbali mbali, ukiwa kama kiongozi
uwe tayari kupokea ushauri ili uweze kuboresha utendaji wako”, amesisitiza Dkt
Ndumbaro.
Dkt Ndumbaro amewaasa
viongozi hao kuwapongeza watumishi wanaofanya kazi kwa bidii na wenye nidhamu
ili iwe motisha kwa wale wavivu huku akiwataka kuwachukulia hatua wale wazembe
na ambao hawataki kufuata kanuni na maadili ya utumishi wa umma.
“Unakuta mtumishi
anajituma anafanya kazi kwa bidii, ana nidhamu na ni mbunifu lakini wewe
kiongozi wake unamuangalia tu bila hata ya kumpongeza, hiyo inakatisha tamaa,
inatakiwa umpongeze sio lazima umpe fedha hata barua tu ya kutambua utendaji
wake itampa hamasa yeye na wenzake. Lakini pia kuna mwingine anakuwa hatekelezi
wajibu wake unamtazama tu, hapo utawakatisha tamaa hata wale wachapakazi,
amesema.
Aidha amewapongeza
watumishi wenye vyeti halali huku akieleza kuwa zoezi la uhakiki wa watumishi
bado ni endelevu ili kuhakikisha watumishi wanaobaki serikalini ni wale
wanaostahili tu huku akiwashauri watumishi kuhakikisha wanasafisha taarifa zao
muhimu ziwe halali na sahihi.
Naye Katibu Tawala
Mkoa wa Singida Dkt. Angelina Mageni Lutambi amemshukuru Katibu Mkuu Utumishi kwa
kuwatembelea watumishi wa Mkoa wa Singida na kusikiliza changamoto pamoja na
maoni yao huku akiahidi kwa niaba ya watumishi kuwa wataendelea kuchapa kazi
kwa bidi na nidhamu.
Dkt Lutambi amesema
watumishi Mkoani Singida wanaadhimisha wiki ya Utumishi wa Umma kwa kufanya
kazi kwa bidi pamoja na kuongeza muda wa kufanya kazi kutoka saa tisa na nusu
mchana mpaka saa kumi na nusu jioni ili kutoa muda zaidi wa kuwahudumia
wananchi.
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Linno Mwageni amemshukuru Katibu
Mkuu Utumishi kuutembelea Mkoa wa Singida na kutoa maoni yake kuwa ili
kuboresha utendaji hasa wa serikali za Mitaa inabidi serikali iwaajiri
watendaji wa vijiji na kata wa kutosha.
Mwageni amesema
watekelezaji wa shughuli na miradi ya serikali kwa ngazi ya mwananchi hasa ni
watendaji wa vijiji na kata ambao kwa sasa ni wachache hivyo serikali iwaajiri
wa kutosha ili waweze kufuatili kwa ukaribu miradi hiyo.
Afisa Elimu Taaluma
Mkoa wa Singida Mwalimu Eva Mosha akitoa maoni yake kwa Katibu Mkuu Ofisi ya
Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma Dkt. Laurean Ndumbaro aliwapotembelea
watumishi wa Mkoa wa Singida katika kuadhimisha wiki ya Utumshi wa Umma.
Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Linno Mwageni akimshukuru Katibu Mkuu Utumishi
kuutembelea Mkoa wa Singida pamoja na kutoa maoni yake ya kuboresha utumishi wa
Umma.
Katibu Mkuu Ofisi ya
Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma Dkt. Laurean Ndumbaro akiandika maoni na
changamoto za watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida (hawapo pichani)
kama sehemu ya maadhimisho ya wiki ya utumishi wa Umma kulia kwake ni Katibu
Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Angelina Mageni Lutambi.
No comments:
Post a Comment