Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt. Rehema Nchimbi akiupokea mwenge wa uhuru kutoka kwa Mkuu wa Mkoa
wa Dodoma Jordan Rugimbana mapema leo katika kijiji cha Sanza Wilayani Manyoni.
Kiongozi wa mbio za
mwenge wa uhuru kitaifa Amour Hamad Amour na mkimbizi mwenge kitaifa Fredrick
Ndahani (ambaye ni mwana Singida) wakiendesha pikipiki zitakazotumiwa na
waratibu wa sekta binafsi mkoani singida wakati wa uzinduzi wa Mkakakti huo.
Kiongozi wa mbio za
mwenge wa uhuru kitaifa Amour Hamad Amour akishona nguo mara baada ya kuzindua
kikundi cha ushonaji katika kijiji cha Nkonko Wilayani Manyoni.
Mwenge wa uhuru leo umezindua
rasmi mkakati wa kuboresha sekta binafsi mkoani Singida kwa kuwa na madawati ya
kuratibu sekta hizo ili kufikia uchumi wa kati wenye viwanda.
Kiongozi wa mbio za
mwenge wa uhuru kitaifa Amour Hamad Amour na mkimbizi mwenge kitaifa Fredrick
Ndahani (ambaye ni mwana Singida) wamezindua mkakati huo kwa kukabidhi pikipiki
mbili kati ya saba kwa maafisa maendeleo ya jamii ambao ndio waratibu wa madawati
hayo.
Akitoa maelezo ya
Mkakati huo mara baada ya kuupokea Mwenge wa Uhuru kutoka Mkoani Dodoma, Mkuu
wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi amesema ushirikiano baina ya serikali na
sekta binafsi utaufikisha Mkoa wa Singida katika azma ya kuwa na uchumi wa kati
pamoja na viwanda.
Dkt Nchimbi amesema
usafiri huo wa pikipiki unalenga kuwawezesha waratibu wa sekta binafsi kila
halmashauri Mkoani Singida kutembelea na kutambua changamoto, fursa na
mafanikio ya sekta binafsi na sio kusubiria ofisini waletewe taarifa au
malalamiko.
“Dawati litatambua
kwa takwimu, mahali, aina ya shughuli na hali ya uzalishaji ili kuhakikisha
ushiriki mtambuka unaowajibika ipasavyo ikiwemo kutoa taarifa ya soko la mazao
mbalimbali. Lengo ni kurahisisha uwekezaji mkoani kwetu”, amesema Dkt. Nchimbi.
Amesema Mkoa wa
Singida unazo fursa za uwekezaji katika viwanda vidogo, vya kati na vikubwa
hasa vitakavyolenga kuongeza thamani ya mazao kutokana na uzalishaji mzuri wa
mazao kama ya vitunguu, alizeti na asali mkoani hapa.
Dkt Nchimbi amesema
sambamba na mkakati huo mwenge wa uhuru umezindua mkakati wa kutunza mazingira
wenye kauli mbiu ya ‘achia shoka kamata mzinga’ ambapo mkoa umetoa mizinga ya
nyuki kwa wachoma mikaa.
Amesema mkakati huo
umewalenga hasa wachoma mikaa ambao wamekiri kuwa waharibifu wa mazingira kwa
kukata miti hovyo hivyo wamekubali kufuga nyuki kwa ajili ya kujitengenezea
kipato cha uhakika huku wakitunza mazingira.
Kwa upande wake
Kiongozi wa Mbio za mwenge wa uhuru kitaifa Amour Hamad Amour ameupongeza
uongozi wa Mkoa wa Singida kwa ubunifu huo unaolenga kuboresha mazingira ya kufanikisha
lengo la kufikia uchumi wa kati na wa viwanda.
Amesema jitihada hizo
za vitendo zinaonyesha wazi ushirikiano mzuri na kudhihirisha namna
wanavyomuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano katika kufanikisha kuinua
uchumi wa taifa.
Aidha amewapongeza
wananchi wa Singida kwa kufanya kazi kwa bidii na kuzalisha mazao ya kutosha,
amewasisitiza kuendelea kumuunga mkono Rais pamoja na kutunza umoja na amani ya
Taifa.
Aidha kiongozi wa
mbio za mwenge wa uhuru Amour Hamad Amour, amefurahishwa na namna wilaya ya
Manyoni ilivyokuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha dhana ya Tanzania ya
viwanda inatekelezwa kwa vitendo.
Amour ametoa pongezi
hizo wakati mwenge ukipita katika miradi mbalimbali wilayani Manyoni huku akiusemea
mradi wa ushonaji nguo na wa ufugaji nyuki kibiashara kuwa ni ishara ya uwepo
wa viwanda vidogo, vya kati na hata vikubwa siku za baadaye wilayani humo.
“Nitumie fursa hii
kuwaomba maafisa wa maendeleo ya jamii, wahakikishe vikundi vya wanawake na
vijana wanapatiwa mikopo kutoka asilimia tano ya mapato ya ndani ya
halmashauiri ili viweze kupata nguvu ya kuanzisha viwanda vidogo. Msiishie
hapo, wapeni na mafunzo mbalimbali ya ufugaji nyuki, kuku na mifugo kibiashara”,
amesema Amour na kuongeza;
“Na hawa akina mama
waliojiunga kwenye kikundi cha ushonaji, wapewe mafunzo ya kuboresha shughuli
zao ziweze kwenda na wakati”.
Mwenge wa uhuru leo
umepokelewa mkoani Singida ukitokea Mkoani Dodoma kupitia kijiji cha Sanza
wilayani Manyoni, mwenge wa uhuru unakimbizwa mkoani Singida katika halmashauri
saba, unakimbizwa kilomita 1064, unatembelea, kuzindua na kufungua jumla ya
miradi 45 yenye thamani ya shilingi bilioni 21.9.
Katibu Tawala Mkoa wa
Singida Dkt Angelina Lutambi akiwa ameubeba mwenge wa uhuru mara baada ya kukabidhiwa
Mkoani Singida Mapema leo katika kijiji cha Sanza Wilayani Manyoni.
Mkimbiza Mwenge kitaifa
Fredrick Ndahani (ambaye ni mwana Singida) akiendesha pikipiki zitakazotumiwa
na waratibu wa sekta binafsi mkoani singida wakati wa uzinduzi wa Mkakati huo.
No comments:
Post a Comment