Friday, February 24, 2017

WANAWAKE ACHENI KULALAMIKA MNA UWEZO WA KUINUA UCHUMI; DKT NCHIMBI.


Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akizindua jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi Mkoani Singida, kulia kwake ni Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Angelina M. Lutambi na kushoto ni Mratibu wa Jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi Mkoani Singida Daniel Munyi.


Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi amewataka akina mama wajasiriamali wote kuacha kulalamika na kutumia fursa zilizopo kujiinua kiuchumi kwakuwa wakati wa kulalamika umeisha na sasa ni kuchapa kazi tu. 

Dkt. Nchimbi ametoa rai hiyo mapema leo wakati akizindua rasmi jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi Mkoa wa Singida na kusisitiza kuwa wanawake sio dhaifu bali watu dhaifu ni wale wanaofikiria mwanamke ni dhaifu. 

Dkt. Nchimbi ameongeza kuwa jukwaa hilo alilolizindua liwe sehemu ya kuwafundisha akina mama mbinu na fursa za uwekezaji pamoja na matumizi mazuri ya fedha wanazozipata hasa mikopo.
Amesema ‘kukopa hakukwepeki katika maisha ya sasa, ila akina mama wengine wanakopa na kuzitumia, vibaya ukiona nguo inapita unanunua wakati haikuwa katika malengo ya mkopo, eti ukishakopa ndio unatamani kula kuku ujionyeshe una pesa, hapana….. kwa namna hii hautaweza kufika popote, hakikisha unabaki katika malengo ya mkopo’.

Dkt. Nchimbi amesema jukwaa liwe jicho la kuhakikisha kuna usalama wa chakula Mkoani Singida kwa kuanzia ngazi ya kila kaya ambapo wanapaswa kuelimisha kaya kuhusu matumizi mazuri ya chakula hasa kulima mazao yanayotumia maji kwa ufanisi na kutunza akiba ya chakula.

Ameeleza kuwa majukumu ya jukwaa hilo ni pamoja na kuangalia namna ya kurejesha maadili ya vijana na kuwakemea ili wasijiingize katika matumizi ya madawa ya kulevya kwakuwa limekuwa tatizo katika maeneo mengi.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi Mkoa wa Singida Bi Neema Salumu ambaye amechaguliwa mara baada ya jukwaa hilo kuzinduliwa amewashuruku wajumbe kwa kumuamini na kumchagua huku akiahidi ushirikiano na kufanya kazi kwa bidii katika kuhakikisha wanawake sehemu ya kukuza uchumi.

Naye Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Angelina M Lutambi amewashukuru wanawake ambao wametoka katika halmashauri zote saba za mkoa wa singida kwa kushiriki uzinduzi wa jukwaa hilo.

Dkt. Lutambi ameongeza kuwa anasimamia na kutekeleza mambo yote yanayohusu maendeleo hasa yanayolenga kuboresha uchumi wa mwanamke Mkoani Singida kwakuwa anaamini ukimuwezesha mwanamke unajenga uchumi wa taifa.

Wajumbe walioshiriki jukwaa la uwezeshaji wanawake uchumi Mkoani Singida wamepewa elimu ya sheria ya kodi na umuhimu wa kulipa kodi, elimu na upatikanaji wa mikopo pamoja na uhusiano wa wanawake na uchumi wa Tanzania.
Baadhi ya wanawake wajasiriamali waliohudhuria uzinduzi wa jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi Mkoani Singida. 
Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Angelina M. Lutambi akizungumza na wanawake wajasiriamali wa Mkoa wa Singida na kushoto kwake ni Mratibu wa Jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi Mkoani Singida Daniel Munyi.

Mwenyekiti wa jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi Mkoani Singida Bi Neema Salumu akiwashukuru wajumbe kwa kumuamini na kumchagua nyuma yake ni Makamu Mwenyekiti wa jukwaa hilo Happy Fransis.
Mwenyekiti wa jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi Mkoani Singida Bi Neema Salumu akiwashukuru wajumbe kwa kumuamini na kumchagua kushoto kwake ni Makamu Mwenyekiti wa jukwaa hilo Happy Fransis na Kulia ni Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Angelina M. Lutambi.

No comments:

Post a Comment