Tuesday, February 14, 2017

MAMA MAGUFULI NA MAMA MAJALIWA WATOA ZAWADI YA TANI SABA ZA CHAKULA KWA WAZEE WA SUKAMAHELA MKOANI SINGIDA.

Mke wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Janeth Magufuli akiwa na Mke wa Waziri Mkuu Mama Mery Majaliwa wakikabidhi zawadi ya chakula kwa wazee na walemavu waishio kambi ya Sukamahela iliyopo wilayani Manyoni, wa kwaza kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Rehema Nchimbi.
Baadhi ya chakula kilichotolewa na Mke wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Janeth Magufuli akiwa na Mke wa Waziri Mkuu Mama Mery Majaliwa kwa wazee na walemavu waishio kambi ya Sukamahela iliyopo wilayani Manyoni, chakula chote kilichotolewa ni tani 7.5 za mahindi, maharage na mchele.


Wazee na walemavu waishio kwenye kambi ya Wazee ya Sukamahela iliyopo Wilayani Manyoni,  Mkoani Singida,  jana 13 Februari 2017,  wametembelewa na Mke wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Mama Janeth Magufuli pamoja na Mke wa Waziri Mkuu Mama Mary Majaliwa na kupokea msaada wa tani 7.5 za vyakula ambavyo ni mchele, unga wa sembe na maharage.

Akikabidhi msaada huo kituoni hapo Mama Janeth amemtaka msimamizi wa kituo hicho Bw. Jeremia Mgoo kuhakikisha chakula hicho kinatumika kwa matumizi yaliyokusudiwa na hakichakachuliwi.

"Viongozi naomba mfuatilie chakula hiki na kuhakikisha kinatunzwa na kutumika vizuri, ili kiwafae Wazee wetu hawa ambao jamii imewasahau, na mimi binafsi jicho langu litakuwa hapa kufuatilia ili kuhakikisha hakichakachuliwi na atakaefanya kinyume tutamshughulikia"  amesema Mama Janeth.

Mke wa Rais pia amewaomba wadau mbali mbali nchini na watu wote wenye mapenzi mema kujitolea kuwasaidia Wazee na watu wasiojiweza waishio katika makambi ya kulelea Wazee kote nchini kwani Wazee hawa ni kundi lililosahaulika na wamekuwa na changamoto zinazofanana ilihali hakuna anaekumbuka kujitolea kuwasaidia hivyo kuishi katika mazingira magumu.

Nae Mama Mary Majaliwa akizungumza kambini hapo amesisitiza wadau mbalimbali kujitokeza na kuwasaidia wazee waishio katika makambi ya kulelea walemavu na wasiojiweza kote nchini.

“Watanzania wajenge tabia ya kuwakumbuka na kuendelea kuwasaidia Wazee hawa kama tulivyofanya sisi ili nao wajisikie kupendwa na wanajamii wenzao” amesema.

Wakati huo huo msimamizi wa Makazi hayo Bw. Jeremia Mgoo amesema kituo hicho kilianzishwa mwaka 1974 chini ya Idara ya Ustawi wa Jamii kwa lengo la kuwasaidia watu wenye ukoma na wazee wasiojiweza mkoani Singida huku akibainisha changamoto zinazokikabili kituo hiko kuwa ni upungufu wa wapishi kwani kituo kinampishi mmoja tu hali inayopelekea Wazee hao kupikiwa mlo mmoja tu kwa siku na uchakavu wa  nyumba wanazoishi Wazee hao. 

Akitoa shukrani zake kwa niaba ya wenzake Mwenyekiti wa Wazee waishio kambini hapo,  Mzee Andrea Yohana ameshukuru kwa msaada huo wa chakula kutoka kwa Mhe. Mama Janeth Magufuli akisindikizwa na Mama Mary Majaliwa na kuwaomba wasichoke kuja kuwaona tena na kuwapa msaada kila wanapojaaliwa. 

Mke wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Janeth Magufuli akiwa na Mke wa Waziri Mkuu Mama Mery Majaliwa wakitembelea makazi ya wazee na walemavu waishio kambi ya Sukamahela iliyopo wilayani Manyoni.
 
Mmoja wa wazee waishio kambi ya Sukamahela akizungumza na Mke wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Janeth Magufuli akiwa na Mke wa Waziri Mkuu Mama Mery Majaliwa baada ya kukabidhi zawadi ya chakula kwa wazee na walemavu waishio kambi ya hiyo iliyopo wilayani Manyoni.

No comments:

Post a Comment