Wednesday, February 08, 2017

MAAFISA UGANI SINGIDA WATAKIWA KUWATEMBELEA NA KUTOA USHAURI KWA WAKULIMA MASHAMBANI

Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dokta Angelina M Lutambi akimkabidhi baiskeli Afisa Ugani wa Kata ya Mwankonko Shilungu Lukanya, baiskeli hiyo imenunuliwa na Mkuu wa Mkoa.

Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dokta Angelina M Lutambi amewataka maafisa ugani kuwatembelea wakulima mashambani na kuwapa ushauri wa kitaalamu juu ya kilimo bora ili wakulima wapate mavuno ya kutosha na kuwa na uhakika wa chakula. 

Dokta Lutambi ameyasema hayo ofisini kwakwe wakati akikabidhi baiskeli yenye thamani ya shilingi laki moja na elfu themanini kwa afisa ugani wa kata ya Mwankonko Bw. Shilungu Lukanya ambapo baiskeli hiyo ilinunuliwa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Rehema Nchimbi.

Amesema Mkuu wa Mkoa alifanya maamuzi ya kumnunulia baiskeli afisa ugani huyo baada ya wanakijiji cha Mwankonko kupongea kazi nzuri ya afisa huyo ya kuwatembelea mashambani na kuwapa ushauri huku wakieleza kuwa changamoto kubwa ya utekelezaji wa majukumu yake ni ukosefu wa usafiri.

Dokta Lutambi amesema baiskeli hiyo aliyopewa na Mkuu wa Mkoa ikawe tija kwake kwa kuongeza juhudi na bidii ya kuwatumikia wakulima kwa kuwatembelea mara kwa mara na kuwapa ushauri na maelekezo yatakayowqeza kuongeza mavuno katika msimu huu.

Ameongeza kuwa utendaji kazi wa afisa ugani huyo aliyepewa baskeli na Mkuu wa Mkoa ukawe chachu na hamasa kwa watendaji wengine ili wajitume kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwakuwa afisa huyo amekuwa mfano kwa kupongezwa na wakulima kwa kuwatumikia vema.

Kwa upande wake Afisa ugani kata ya mwankonko Shilungu Lukanya amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Rehema Nchimbi kwa kumpatia usafiri huo utakaomuwezesha kutembelea mashamba mengi zaidi na kwa muda mfupi.

Lukanya amesema katika kata ya Mwankonko wakulima wengi wamelima mazao yanayotumia maji kwa ufanisi kama vile mihogo ambapo kila kaya imehamasika kulima nusu ekari ya zao hilo.

Amesema katika kata hiyo chakula kipo na kuna uhakika wa mavuno mazuri endapo mvua zitaendelea kunyesha huku akieleza kuwa elimu inaendelea kutolewa kwa wakulima juu ya kuhifandhi chakula baada ya mavuno ili wasikitumie vibaya mara baada ya mavuno.
Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dokta Angelina M Lutambi akimkabidhi baiskeli Afisa Ugani wa Kata ya Mwankonko Shilungu Lukanya, baiskeli hiyo imenunuliwa na Mkuu wa Mkoa.

Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dokta Angelina M Lutambi akimkabidhi baiskeli Afisa Ugani wa Kata ya Mwankonko Shilungu Lukanya, baiskeli hiyo imenunuliwa na Mkuu wa Mkoa.

No comments:

Post a Comment