Friday, January 27, 2017

MANISPAA YA SINGIDA YAPEWA MWEZI MMOJA MRADI WA MAJI KISASIDA UANZE KUFANYA KAZI.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi ameziagiza halmashauri ya Manispaa, ihakikishe ndani ya mwezi moja kuanzia sasa skimu ya umwagiliaji ya kijiji cha Kisassida inaanza kufanya kazi iliyokusudiwa.

Dkt. Nchimbi ametoa agizo hilo juzi akiwa kwenye  ziara yake ya siku moja ya kukagua na kuhamasisha shughuli za kilimo katika  vijiji vya  manispaa ya Singida.

Amesema ni jambo la kusikitisha mno kuona skimu  hiyo ambayo ujenzi wake umekamilika kujengwa mwaka 2015 kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 750 lakini hadi sasa mradi huo haujaanza kufanya kazi kwa kukosa nishati ya umeme.
  
“Kilimo cha umwagiliaji ndicho kinachopewa kipaumbele na serikali ya awamu ya tano haina urafiki na uzembe wa aina hii. Hebu  angalieni anga lote lilivyo  jeupe,  mradi huu ungekuwa umesimamiwa vizuri, wakazi zaidi ya 3,000 wa kijiji cha Kisasida na manispaa kwa ujumla,  wangekuwa  na uhakikia wa chakula na hali zao za  kiuchumi,  zingekuwa nzuri”, amesema.

Dkt. Nchimbi ametoa siku saba awe amepata taarifa kamili ya mradi huo huku akionyesha kusikitishwa na kutoanza kufanya kazi kwa mradi huo kwa wakati ilihali  miundimbinu  yote muhimu ikiwemo mabomba ya kunyunyuzia  maji yakiwa yapo.

“Kipindi cha mwaka miwili manispaa ya Singida imeshindwa kuunganisha umeme kwenye skimu hii, hili ni jambo la kusikitisha. Huko nyuma zilihitajika shilingi 128 milioni tu kuvuta umeme ikashindikana sasa zinahitajika zaidi ya shilingi 300 milioni, ninachotaka ni kwamba ndani ya mwezi moja skimu hii ianze kazi”, ameongeza.

Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa Dkt. Nchimbi, ametumia fursa hiyo kutembelea na kugakua shughuli za kilimo cha kisasa anachofanya mkulima Hassan Tati ambaye analima na kufuga kisasa.

Dkt. Nchimbi amempongeza Tati kwa shughuli hizo za kilimo na ufugaji wa kisasa huku akiwahamasisha vijana kuiga mfanoi wa mkulima huyo kuliko kuliko kusubiri ajira.

“Serikali ya mkoa inataka kuona wananchi na hasa vijana wengi  wakiiga mfano kutoka Kwa Tati kwa kulima na kufuga  kwa bidii na maarifa, ili mkoa uwe na chakula cha kutosha na kupata zaida kwa ajili ya kulisha makao makuu ya nchi pale Dodoma”, ameongeza Dk.Nchimbi.

Katika maonyesho ya wakulima na wafugaji ya nanenane mwaka jana Mkulima Tati alikua mshindi wa kwanza kanda ya kati katika ufugaji na mshindi wa pili kikanda katika kilimo.

No comments:

Post a Comment