Friday, December 16, 2016

RC NCHIMBI ALIPONGEZA SHIRIKA LA NYUMBA; AZUNGUMZA NA WATUMISHI MANYONI NA KUWAKUMBUSHA MAADILI YA UTUMISHI WA UMMA.



Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akizungumza na watumishi wa halmasahuri ya Wilaya ya Manyoni pamoja na mambo mengine amewataka watumishi hao kubadilika ili waweze kwenda sambamba na dhana ya serikali ya hapa ni kazi tu.





Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akikabidhiwa na Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa NHC Mkoa wa Singida Ladislaus Bamanyisa (kulia) msaada wa vifaa vya ujenzi kwa ajili ya bweni la sekondari Mwanzi iliyoko Wilaya ya Manyoni, bweni moja la wasichana liliteketezwa kwa moto mwezi Septemba mwaka huu. 
 


Baadhi ya watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Manyoni Mkoani Singida wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa Dkt. Rehema Nchimbi kwenye mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo.




Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akizungumza na watumishi wa halmasahuri ya Wilaya ya Manyoni pamoja na mambo mengine amewataka watumishi hao kubadilika ili waweze kwenda sambamba na dhana ya serikali ya hapa ni kazi tu.
 
Mkuu  wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi amelishukuru Shirika la Nyumba  Taifa (NHC) kwa msaada wa mifuko ya saruji 10, kofia za bati 20, mabati 90 ya geji 28 vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi 2.6 milioni ukiwa ni msaada kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa bweni la sekondari Mwanzi iliyoko Wilayani Manyoni Mkoani Singida.
 
Dkt. Nchimbi ametoa shukrani hizo juzi wakati akipokea masaada huo kutoka kwa Meneja wa NHC Mkoa wa Singida Ladislaus Bamanyisa na kutoa wito kwa mashirika, watu binafsi na taasisi zikiwemo mabenki, kuiga mfano mzuri wa NHC kusaidia serikali katika kuboresha sekta mbalimbali ikiwemo ya elimu.
 
“Mimi nitumie nafasi hii kuwaita au kuwaalika mabenki na taasisi zingine kuja mkoani Singida kutuunga mkono katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi, pamoja na uboreshaji wa miundo mbinu ya shule za msingi na sekondari”,amesema.
 
Ameongeza kuwa benki, shirika au watu binafsi watakaojitokeza kuunga mkono kuuendeleza Mkoa wa Singida kwa kujenga jengo lo lote pamoja na majengo ya shule, huduma za afya na mengine yanayolenga kuwanufaisha wananchi, wataruhusiwa kupaka rangi na kuweka nembo zao ili kutangaza shughuli au huduma wanazotoa.
 
Amesema kwa njia hiyo benki, taasisi au watu binafsi watakuwa wamejitangaza na tangazo hilo litadumu kwa muda mrefu ikilinganishwa na matangazo mengine.
 
“Kwa upande wa wadau binafsi na wao wataruhusiwa kuweka picha za familia zao kwenye majengo au miradi husika. Kama ni mfugaji na ameuza sehemu ya mifugo yake kugharamia miradi wa umma, ataruhusiwa kuweka picha ya familia na ng’ombe zao”, amesema Dkt. Nchimbi.
 
Naye Meneja wa NHC Mkoa wa Singida Ladislaus Bamanyisa, amesema wataendelea kuiunga mkono serikali katika kuboresha sekta mbalimbali na huo mchango ni sehemu ndogo ambapo shirika bado linaendele ana jitihada za kukusanya michango mingine.

Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Nchimbi amezungumza na watumishi wa halmashauri ya Wilaya ya Manyoni na kuwaeleza kuwa halmashauri za wilaya na manispaa zimekuwa ni chanzo au viwanda vya kuzalisha mabango na kelele nyingi kwa wananchi kutokana na huduma zisizokidhi mahitaji na ubadhirifu wa fedha za umma.
 
Dkt. Nchimbi ameongeza kuwa ataelekeza nguvu zake kuanzisha na kufufua kilimo cha umwangiliaji na ufugaji wa samaki ili Mkoa uweze kunufaika kiuchumi na ujio wa makao makuu kuhamia mkoa jirani wa Dodoma.
 
“Sisi wakazi wa mkoa wa Singida sote ni lazima tujiandae kikamilifu kulisha makao makuu ya nchi yatakapokuwa Dodoma. Tuitumie fursa hiyo kumtokomeza adui umaskini”, amesisitiza.
 
Naye Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Geofrey Mwambe amesema wakati wanaendelea na ujenzi wa bweni halmashauri ya Manyoni imejipanga pia kujenga uzio katika shule hiyo ya sekondari ya Mwanzi ili kuboresha ulinzi katika shule hiyo.
 
Mwambe amesema kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wanamalizia ujenzi wa bweni moja na kuanza ujenzi wa bweni lingine huku akiwashukuru wafanyabiashara wa Wilaya ya Manyoni kwa kujitoa katika kusaidia maendeleo ya Wilaya hiyo.

 Picha na Gasper Andrew

No comments:

Post a Comment