Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Rehema Nchimbi akionyesha mbegu bora ya muhogo aina ya Momba inayozalishwa katika shamba la Mpambaa halmashauri ya Singida, katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Singida Elias Tarimo na anayefuata ni Afisa Kilimo halmashauri ya Singida Abel Mungale.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Rehema Nchimbi akiandaa mashimo ya kupanda mbegu bora ya
mbaazi inayozalishwa katika shamba la Mpambaa halmashauri
ya Singida.
Watumishi wa
halmashauri zote saba za Mkoa wa Singida wameagizwa kulima nusu ekari ya mazao
yanayotumia maji kwa ufanisi hasa zao la muhogo, viazi au mtama ili kuwa na
uhakika wa chakula cha kutosha msimu ujao huku shule zote zikiagizwa kulima
ekari moja ya mihogo au mtama ili wanafunzi wapate chakula shuleni.
Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dokta Rehema Nchimi ametoa agizo hilo alipotembelea na kuzindua shamba
la mbegu bora ya mihogo la ekari kumi lililopo kijiji cha Mpambaa, Halmashauri
ya Singida ambalo litazalisha mbegu kwa ajili ya wakulima wa Mkoa wa Singida.
Dokta Nchimbi
ametumia kauli mbiu ya kuongoza ni kuonyesha njia kwa kulima mihogo shamba lake
mwenyewe lenye ukubwa wa ekari tatuna hivyo kuwaagiza watumishi na viongozi
wote kuonyesha mfano kwa kulima mazao hayo kwa msimu huu.
Pamoja na upandaji wa
mbegu za Muhogo, Dokta Nchimbi pia amezindua shamba la mbegu bora za mbaazi kwa
kupanda mbegu hizo pamoja na kupalilia shamba la mbegu bora za mtama ambapo
aina 25 za mtama zinafanyiwa majaribio ili kupata mbegu itakayofaa kwa mkoa wa
Singida.
Aidha ametembelea mashamba
ya wakulima wa mtama wa halmashauri ya Wilaya ya Ikungi pamoja na kushiriki
upandaji wa mtama wa shamba la shule ya Msingi Mampanta wilayani Iramba na
kupanda viazi na mihogo katika shamba la Mkulima wa Old Kiomboi wilayani Iramba.
Amesema wakulima
wakielimishwa juu ya mazao yanayotumia maji kwa ufanisi watapanda mazao hayo
ambayo ni mtama, viazi, muhogo na mbaazi ambapo wakulima watakuwa na uhakika wa
chakula pamoja na kujipatia fedha kwa kuuza mazao hayo.
Dokta Nchimbi ametoa
hamasa kwa wakulima wote kulima mazao hayo yanayotumia maji kwa ufanisi na
wajitume kwa bidii kuliko kulalamikia serikali bila kufanya kazi kwakuwa awamu
ya sasa ya uongozi ni ya kuchapa kazi kwa bidii.
Wakati huo huo Dokta
Nchimbi amefanya vikao na watumishi wa halmashauri za Singida, Ikungi na Iramba
mara baada ya kutembelea mashamba ya wakulima na kushiriki nao katika kupanda
mtama, kupalilia baadhi ya mashamba, kupandqa mihogo na viazi.
Dokta Nchimbi
amewaasa watumishi wote Mkoani Singida kuwa waadilifu, wachape kazi na hasa
kulima mazao yanayotumia maji kwa ufanisi pamoja na kufanya shughuli nyingine
za kuwaingizia kipato kama vile kufuga kuku na kuwa na mizinga ya nyuki ili
wawe na kipato kingine nje ya mshahara.
Amesema watumishi
wengine hujiingiza kwenye wizi kutokana na tamaa tu ila endapo watakuwa na
vyanzo vingine vya fedha nje ya mshahara itapunguza kutokuwa waaminifu pamoja
na kutokulalamika mara kwa mara.
Baadhi ya watumishi
waliohudhuria vikao hivyo wamempongeza Mkuu wa Mkoa Dokta Nchimbi kwa nasaha
alizowapa huku wakiahidi kuchapa kazi kwa bidii na uadilifu pamoja
wakijishughulisha na kilimo ili wawe na kipato cha ziada.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Rehema Nchimbi akipamba mbegu bora ya mbaazi inayozalishwa katika shamba la Mpambaa halmashauri
ya Singida, anayefuata ni Mwenyekiti wa halmashauri ya Singida Eliya Digha.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Rehema Nchimbi akiwaonyesha watumishi wa halmashauri namna ya kupanda mbegu bora ya mbaazi katika shamba la Mpambaa halmashauri
ya Singida.
Watumishi wa halmashauri
ya Singida wakizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Rehema Nchimbi (hayupo pichani).
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Rehema Nchimbi akipanda viazi lishe na mihogo katika shamba la mkulima bora wa eneo la Old Kiomboi Wilayani Iramba.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Rehema Nchimbi akipanda mtama katika shule ya Msingi Mampanta Wilayani Iramba.
No comments:
Post a Comment