Monday, November 28, 2016

WANANCHI WA KITARAKA SINGIDA WAOMBA MAENEO YA UKULIMA NA UFUGAJI



Wananchi wa Kata ya Kitaraka iliyopo katika Halmashauri ya Itigi, Wilaya ya Manyoni, Mkoani Singida, wamemuomba Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mh. William Ole Nasha, kuwapatia shamba linalomilikiwa na Serikali la Tanganyika Packers, ambalo Serikali imeacha kulitumia kwa zaidi ya miaka 20, ili walitumie kwa shughuli za Kilimo na Ufugaji.

Wananchi hao wamefikisha maombi hayo kwa Mh. Waziri alipotembelea shamba hilo lenye ukubwa wa ekari 45,000, na kuzungumza na Wananchi wa Kata hiyo waliolalamika kuwa hawana eneo la kulima wala kufuga ilihali shamba hilo halitumiki na linafaa kwa shughuli hizo.

Nae Mh. Waziri akizungumza na Wananchi hao amesema Serikali ya awamu ya tano ni Serikali inayosikiliza kero za Wananchi na kuzishughulikia kwani ipo karibu zaidi na Wananchi na ndio sababu ya yeye kufika Kijijini hapo ili kuona namna bora ya kutatua changamoto hiyo na kuweka utaratibu jinsi shamba hilo litakavyotumika.

"Wizara inalichukua suala hili ikalitolee maamuzi, Wananchi wavute subira wakingoja Serikali itoe ufafanuzi juu ya suala hili, ni marufuku mwananchi yeyote kuvamia na kufanya shughuli za kilimo ama ufugaji kwa sasa hadi hapo Serikali itakapotoa maelekezo mapya" alisema Mh. Nasha.

Mh. Waziri pia akatoa wito kwa wafugaji wa maeneo hayo kuacha tabia ya kukata miti hovyo, kwani kwa kufanya hivyo kwani wanaharibu mazingira na watapelekea eneo lake kuwa jangwa, akawasisitiza kufuga ufugaji wa kisasa kwa kufuga madume ya kisasa, kupunguza wingi wa mifugo ili uendane na malisho waliyonayo, ukubwa wa eneo na kuendana na mabadiliko ya tabia nchi, kuitumia mifugo yao kujiendeleza kiuchumi kama kuwasaidia kujenga makazi bora na kushiriki kuchangia shughuli za maendeleo.

No comments:

Post a Comment