Viongozi wa
Vijiji kwa kushirikiana na Wananchi pamoja na wadau wa maendeleo, wametakiwa
kujijengea tabia ya kuchangia shughuli za maendeleo katika maeneo yao.
Rai hiyo
ilitolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Mh. Geoffrey Idelphonce Mwambe
alipokuwa akizungumza katika Mkutano na WanaKijiji wa Kata ya Maweni ambapo
alivitembelea Vijiji vya Ngaiti, Mvumi na Maweni akiwa katika ziara ya
kujitambulisha kwa Wananchi na kuhamasisha Wananchi kuchangia shughuli za
maendeleo katika Kata hiyo.
"Nawapongeza sana
Wananchi wa Kata hii kwa juhudi mnazofanya kuchangia shughuli za
maendeleo hasa katika Sekta ya elimu, kwani mmejitahidi kuchangishana na
kufanikiwa kujenga jengo la madarasa mawili
ya shule mpya ya msingi Ighose kwenye kijiji cha Ngaiti na nyumba ya walimu ambazo
zimefikia katika hatua ya kupauliwa, na hii
itasaidia kupunguza adha ya walimu kuishi mbali na maeneo ya shule na hivyo
kuongeza morali wa kufundisha hivyo kuongeza ufaulu wa wanafunzi, hivyo basi, kwa
kuonesha juhudi hizi, Ofisi ya Mkurugenzi ni muda Muafaka sasa kuwaunga mkono
Wanakijiji hawa kuwasaidia kumalizia kupaua majengo haya, ili yaanze kutumika
mapema mwakani shule zitakapofunguliwa" Alisema Mwambe.
Nae Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Manyoni, Bw. Charles
E. Fussi akizungumza katika mkutano huo
amewataka Watendaji wa Kata na Vijiji, wazazi, Wenyeviti wa bodi za Shule
na kamati za Shule kuwa mfano kwa kuwa mstari wa mbele kuchangia
shughuli za maendeleo hasa elimu, katika kupambana na adui ujinga ili kizazi
kijacho kiwe na maendeleo stahiki.
Diwani wa Kata
hiyo ya Maweni Mh. Abdul Mwengwa amemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kufanya ziara
katika Kata yake kwani imeamsha ari ya Wananchi kushiriki na kuchangia shughuli
za maendeleo hasa ikizingatiwa sasa wako katika kuhamasisha Wananchi kuchangia
ujenzi wa Zahanati yao ya Maweni na kutumia fursa hiyo kuwaomba wadau
mbalimbali wa maendeleo kuwasaidia misaada ya hali na mali kukamilisha ujenzi
wa Zahanati hiyo ili waondokane na adha wanayoipata sasa ya kukosa huduma za
afya.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa
Wilaya amewapongeza Wananchi wa Kata ya Chikuyu kwa kufanikisha ujenzi wa shule
ya msingi Chilejeho, iliyopo kata ya Chikuyu ambayo inahitaji bati 25 na mifuko
50 ya saruji kukamilika, ili watoto waanze kuyatumia madarasa hayo ifikapo Januari
mwakani.
Mkuu wa wilaya alipita kijijini
Chilejeho Kata ya Chikuyu, akiwa njiani kutoka kwenye ziara ya siku nzima
aliyoifanya kwenye Kata ya Maweni, ambapo alitumia fursa hiyo kuwaasa wazazi
kuacha kulichukulia suala la elimu kimzaha wakati Serikali ya Awamu ya tano
imedhamiria kutoa elimu bure kuanzia chekechea hadi Sekondari.
No comments:
Post a Comment