Mwenyekiti wa Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew John Mtigumwe akiongoza kikao hicho, kushoto kwake ni Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dokta Angelina Mageni Lutambi, wa kwanza kulia ni Waziri wa Mambo ya ndani Mwigulu Lameck Nchemba na anayefuata ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida Mhe. Martha Mlata.
Mbunge wa Viti maalum CCM Singida Aisharose Matembe akichangia hoja katika kikao cha kamati ya ushauri ya Mkoa wa Singida (RCC).
Meneja wa SIDO Mkoa wa Singida Shoma Kibende akichangia hoja katika kikao cha kamati ya ushauri ya Mkoa wa Singida (RCC).
Na Nathaniel Limu-Singida.
Wafanyabiashara wa kuku wa
asili/kienyeji mkoani Singida wamejipatia mapato ya zaidi ya shilingi bilioni
1.8, baada ya kuuza kuku 151,242 katika kipindi cha mwaka jana hadi sasa.
Hayo yamesemwa juzi na kaimu Katibu
Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji Beatus Choaji wakati akitoa taarifa ya
uendelezaji wa kuku wa asili, kwenye kikao cha kamati ya ushauri mkoa (RCC) kilichofanyika
kwenye ukumbi wa mikutano uliopo kwenye jengo la ofisi ya mkuu wa mkoa mjini
hapa.
Chowaji amesema mapato hayo
yamepatikana baada ya kuku hao 151,242 kusafirishwa na kuuzwa nje ya mkoa ikiwemo jijini
Dar-es-salaam.
“Kuku wa asili wakifungwa vizuri
kwa kudhibiti ugonjwa wa mdondo na kuzingatia kanuni za ufugaji bora wanaweza
kuleta mabadiliko makubwa na ya haraka ya kipato. Kuku wa asili pia ni lishe bora
hususani kwa watoto na akina mama”, ameongeza Choaji.
Ili kuimarisha ufugaji kuku wa
asili amesema imependekezwa halmashauri zote zitekeleze mkakati wa kuchanja
kuku kwa wakati moja mara tatu kwa mwaka kwa kutumia watoa chanjo wasiokuwa
wataalam wa mifugo.
Akisisitiza amesema “Mkakati huu
unatarajiwa kuanza mara halmashauri zitakazokamilisha utoaji wa mafunzo kwa
watoa chanjo hao. Halmashauri zimesisitizwa kushiriki kikamilifu kutekeleza mkakati
huo ili kuinua kipato cha wananchi kwa haraka zaidi”.
Mapema Mkuu wa Mkoa wa Singida na
mwenyekiti wa kikao hicho, Mhandisi Mathew John Mtigumwe, akifungua kikao hicho
ameagiza kuwa wananchi wahamasishwe, ili wasiendelee kuuza chakula walichovuna
msimu uliopita kiweze kuwafikisha msimu ujao wa mavuno.
Mhandisi Mitugumwe amesema kwa
mujibu wa mamlaka ya hali ya hewa nchini (TMA) mvua za msimu huu zinatarajiwa
kunyesha kwa kiwango cha chini ya wastani.
“Hivyo ni jukumu letu sote kuhimiza
na kushauri wananchi kufuata kanuni bora za kilimo na kupanda mazo ya
kipaumbele yanayostahimili ukame, na yanayokomaa mwa muda mfupi.
Wakati huo huo Mkuu huyo wa mkoa,
ametumia fursa hiyo kutoa shukrani zake za dhati kwa wananchi wadau wa elimu, wafanyabiashara,
kampuni za simu za viganjani na mashirika ya umma na binafsi, kwa kushiriki
kutekeleza agizo la rais Magufuli la kumaliza uhaba wa madawati mashuleni.
No comments:
Post a Comment