Mwenyekiti wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Anne Makinda akikagua hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Singida, mwenye tai nyekundu ni Mkuu wa Mkoa wa Singida Mheshimiwa Mhandisi Mathew John Mtigumwe.
Mwenyekiti
wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Anne Makinda akikagua
hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Singida,kulia kwake ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dokta Ramadhani Kabala na kushoto ni Mkuu wa
Mkoa wa Singida Mheshimiwa Mhandisi Mathew John Mtigumwe.
Mwenyekiti wa bodi ya
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Anne Makinda amezishauri hospitali, vituo
vya afya na zahanati za serikali kuboresha huduma za afya ili wananchi
waliojiunga katika mifuko ya afya ya jamii (CHF) na mfuko wa bima ya afya washawishike
kutumia huduma katika hospitali zao.
Makinda ametoa rai
hiyo alipotembelea hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida kujionea huduma za
Bima ya afya zinavyotolewa na changamoto zilizopo ili kwa ushirikiano wa mfuko
wa bima ya afya na wadau wake waweze kuzitatua.
Amesema hospitali na
vituo binafsi au vya mashirika mbalimbali wamekuwa wanufaikaji wakubwa wa
kupata wateja wengi wa bima ya afya na mifuko ya afya ya jamii kutokana na
kusifiwa kuwa wanatoa huduma bora tofauti na hospitali za serikali ambazo
hupata wateja wachache na hivyo kupata faida kidogo.
Makinda amesema
hamasa anayoitoa ya kuboresha huduma kwa vituo vya serikali haimaanishi mfuko
wa taifa wa bima ya afya hauthamini vituo na hospitali binafsi bali inataka
hospitali za serikali kuboresha huduma na kuingia katika ushindani.
Ameongeza kuwa changamoto
ya ukosefu wa dawa na vifaa tiba inawakatisha tamaa watumiaji wa bima ya afya
pamoja na watu wengine kujiunga hata hivyo mfuko wa bima ya afya na hospitali za
serikali zimejipanga kuziondoa changamoto hizo.
Aidha Makinda
ameupongeza Mkoa wa Singida kwa kufanya vizuri katika mfuko wa afya jamii na
bima ya afya huku akisisitiza kuendelea kuboresha ili Mkoa wa Singida uwe mfano kwa mikoa
mingine ya Tanzania.
Akitembelea majengo mapya
ya hospitali rufaa iliyopo eneo la Mandewa Makinda amevutiwa sana na majengo hayo
huku akiutaka uongozi wa Mkoa kwa kushirikia na wadau wengine hasa mfuko wa
bima ya afya kutafuta pesa za ukamilishaji wa majengo muhimu ili huduma zianze
kutolewa katika hospitali hiyo kwakuwa itakuwa msaada hata kwa kanda nzima ya
kati.
Naye Mkuu wa Mkoa wa
Singida Mheshimiwa Mhandisi Mathew J Mtigumwe amemshukuru Anne Makinda kwa
kuutembelea mkoa wa Singida ili kujionea huduma za Bima ya afya zinavyotolewa.
Mheshimiwa Mhandisi
Mtigumwe amemuahidi Makinda kuwa Mkoa utaendeleza ushirikiano mzuri na Mfuko
huo na kuomba waendelee kutoa ushirikiano wa vifaa tiba na ukarabati wa
miundombinu ya hospitali na vituo vya afya vya serikali ili kuboresha huduma za
afya Mkoani Singida.
Ameongeza kuwa Mkoa
utaendelea kuhamasisha wananchi kujiunga na mfuko wa afya ya jamii na bima ya
afya ili wapate huduma bora hata wakati wakiwa na upungufu wa fedha kwani bima
huokoa maisha.
Mwenyekiti
wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Anne Makinda katikati kulia kwake ni Mkuu wa
Mkoa wa Singida Mheshimiwa Mhandisi Mtahew John Mtigumwe na kushoto kwake ni Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dokta Angelina Mageni Lutambi na Mkuu wa Wilaya ya Singida Elias Tarimo, wa kwanza kulia ni meneja Mfuko wa Bima ya Tifa Mkoa wa Singida Bwana Adamu Salumu .
No comments:
Post a Comment