Wednesday, October 12, 2016

WANANCHI WAPEWE ELIMU JUU YA MADHARA YA UCHAFU KIUCHUMI NA KIAFYA.








Mwakilishi Katibu Tawala Mkoa wa Singida Bw. Boniface Temba (katikati) akiwa katika kikao cha wadau wa maji kuhusu kuhusu kuhuisha mipango ya maji Mkoa, Kulia kwake ni Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Mkoa Dokta Abdalah Dihenda na kushoto kwake ni Mhandisi wa Maji kutoka Sekretariet ya Mkoa Emaeli Nkopi.




Serikali na wadau mbalimbali wanatakiwa kuunganisha nguvu na kuzielekeza katika kuelimisha jamii juu ya athari za uchafu ili wahamasike na kuupinga kwa kujenga vyoo bora, kutumia maji safi na salama na kutumia huduma za usafi wa mazingira.

Ari hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Mpango wa ‘Water Aid’ Tanzania Bw. Abel Dugange wakati wa kikao cha wadau wa maji wakati wa kuhuisha mipango ya sekta ya maji ya Mkoa wa Singida.

Dugange amesema nguvu kubwa inatakiwa ielekezwe katika kutoa elimu kwa jamii ili wajenge vyoo bora na kuvitumia, watumie maji safi na salama ili kujiepusha na magonjwa mbalimbali yatokanayo na uchafu.

Ameongeza kuwa serikali inapoteza fedha nyingi katika kuwatibu wananchi wanaogua magonjwa kama kipindupindu, kuhara pamoja na ukusanyaji na utekezaji wa uchafu huku wananchi pia hupoteza pesa kwa kujitibu huku wakipoteza muda wa kuzalisha mali kwenye matibabu.
Dugange amesema mpango wa ‘Water Aid’ kwa mwaka 2016 mpaka 2020 utalenga kuunganisha nguvu na kusaidiana na halmashauri katika kutekeleza mipango yao ya sekta ya maji na usafi wa mazingira ili kufikia malengo ya kitaifa katika sekta hiyo.

Amesema kwa tafiti za mwaka 2015 zinaonyesha kuwa asilimia 58 ya watanzania hupata na kutumia maji safi na salama huku asilimia 18 tu hutumia huduma za usafi wa mazingira.

Dugange amesema kwa upande wa upatikanaji na matumizi ya vyoo bora vya kwa Mkoa wa Singida mijini ni asilimia 31 wakati vijijini ni asilimia nane.

Katika majadiliano hayo wahandisi wa maji na maafisa mazingira wa halmashauri walitoa changamoto za sekta hizo kuwa ni pamoja na ukosefu wa vifaa hasa vya usafiri wa kutembelea na kukagua maeneo mbalimbali.

Changamoto nyingine ni pamoja na visima vingi vya vijijini kuchimbwa maeneo ya mashamba ya wanakijiji ambapo hawalipwi fidia na kusababisha uharibifu wa vyanzo na visima vya maji hasa ukataji wa miti.

Kumekuwepo na wizi wa vifaa katika miradi ya maji hasa solar huku wanakijiji wakiomba kuwekewa umeme wakati utunzaji wa miradi hiyo wakishindwa kuchangia huduma hizo.

Kwa pamoja wadau wamekubaliana kuunganisha nguvu katika kutatua kero za upatikanaji wa maji pamoja na kuboresha usafi wa mazingira.


















Kikao cha wadau wa maji Mkoa wa Singida kikiendelea mweye tai nyekundu ni Afisa Afya Mkoa wa Singida Habib  akiwa na kushoto kwake ni mkurugenzi wa mpango wa Water Aid Tanzania Abel Dugange.

















Wadau wa Maji Mkoa wa Singida wakiendelea na kikao.
 Wadau wa Maji Mkoa wa Singida wakiendelea na kikao.

No comments:

Post a Comment