Monday, June 13, 2016

ZIARANI MKOANI SINGIDA; WAZIRI MBARAWA ATOA MAAGIZO KUHUSU KITUO CHA KUHIFADHIA KUMBUKUMBU

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (wa kwanza kushoto) akipewa maelezo juu ya mitambo ya simu ya TTCL wakati wa ziara yake Mkoani Singida.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbawara ameagiza kituo cha kuhifadhi kumbukumbu mbalimbali (Data centre) cha Kijitonyama jijini Dar-es-salaam kianze kufanya kazi mara moja, kwa madai kituo hicho muhimu kikiendelea bila kufanya kazi, kinaitia hasara kubwa serikali.

Waziri huyo ametoa agizo hilo akiwa ziarani Mkoani Singida akikagua njia ya mkongo wa taifa eno la kijiji cha Iguguno wilaya ya Mkalama, Singida.

Amesema kituo hicho kwa sasa kinaendelea kuitia hasara serikali kwa kuingia gharama mbalimbali ikiwemo ya umeme na mishahara ya wafanyakazi kutokana na kutokuanza kazi, wakati ujenzi wake umekalimila kwa mda mrefu.

“Sielewi kuna sababu gani inakwamisha kituo hicho kuanza kazi wakati wateja wake wako wengi, na wanasubiri tu kituo kianze kufanya kazi. Pengine ni watumishi wake wanafanya kazi kwa mazoea"amesema huku akisisitiza kuwa kituo hicho ni kitega uchumi kikubwa cha serikali.

Kituo hicho ambacho karibu kila nchi duniani inacho, kinatarajiwa kuweka au kuhifadhi taarifa na kumbukumbu mbalimbali muhimu za taasisi za fedha, makampuni na wadau ili endapo taasisi itapoteza taarifa zake muhimu ikiwemo majengo kuugua moto wanaweze kuzipata kwenye kituo hicho.

Katika hatua nyingine, Meneja wa TTCL Kanda ya Kati Peter Lusama amesema kampuni ya simu Tanzania (TTCL) Mkoa wa Singida imekusanya mapato yake zaidi ya shilingi 132 milioni sawa na asilimia 180 ya lengo kati ya Januari hadi Mei mwaka huu.

Lusama amesema mafanikio hayo yametokana na malipo mbalimbali kutoka kwa wateja 4,452 ambapo wateja 1,490 ni wa simu za mezani, 2,932 wa simu za mkononi na wateja 30 walioungwa kupitia mkongo wa Taifa.

“Tukiangalia mwenendo wa mahitaji ya huduma  katika mkongo wa Satellite (Broad band) hasa mradi wa simu za mkononi unaotarajiwa  kuwa tayari mwezi huu wa Juni, tuna uhakika wa kuyapandisha mapato na kuweza kufikia lengo la mwaka huu, la zaidi ya shilingi 232.5 milioni,” amesema.

Aidha, Lusama amesema kama ilivyo kwa Mikoa mingine Singida nayo inapata mawasiliano kupitia katika mkongo wa Taifa wenye urefu wa takribani Kilometa 433.
 
“Kati ya Kilometa hizo 433, Kilometa 153 zimechimbiwa chini ya ardhi na Kilometa 280 zinapita juu ya nguzo za TANESCO. Tunaendelea kutoa elimu kwa wadau wote wa vijiji vinavyopitiwa na mkongo wa Taifa, ili waendelea kuhakikisha usalama wa mkongo unadumishwa,” ameongeza.

TTCL Mkoa wa Singida, inahudumia Wilaya tatu kati ya tano zilizopo. Wilaya hizo ni Singida, Manyoni na Iramba, utoaji wa huduma katika wilaya mpya za Ikungi na Mkalama ziko katika hatua za awali za ujenzi wa minara.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akizungumza na viongozi wa Mkoani Singida akiwa katika ziara yake Mkoani Singida.



Picha/Maelezo  na Nathaniel Limu, Singida.

No comments:

Post a Comment