Wednesday, June 15, 2016

HELVETAS WAJENGA KIWANDA CHA KUSINDIKA MAZAO YA MBOGAMBOGA NA MATUNDA CHA SHILINGI MILIONI 54.





Meneja Mradi wa EU KUWAKI na Shirika la Helvetas Mkoani Singida Andrew Rwechungura akizugumza katika kikao cha wadau wa kilimo cha mbogamboga.
Shirika lisilo la kiserikali la Helvetas chini ya Mradi wa Kuwawezesha Wanawake katika Kilimo cha Mbogamboga (EU KUWAKI)  kwa kushirikiana na serikali na wakulima linajenga viwanda vitatu vya kusindika mazao ya mboga mboga na matunda katika halmashauri za Mkalama, Iramba na Manyoni.

Katika Halmashauri ya Mkalama Helvetas wametoa shilingi milioni 54 kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda hicho katika kijiji cha Gumanga huku halmashauri ya wilaya ya Mkalama ikichangia shilingi milioni tatu na nguvu za wakulima zikiwa na gharama ya shilingi milioni mbili.

Akisoma taarifa ya maendeleo ya  mradi huo katika kikao cha wadau wa kilimo cha mboga mboga na matunda Meneja Mradi wa EU KUWAKI na Shirika la Helvetas Mkoani Singida Andrew Rwechungura  amesema kiwanda hicho kitasaidia wakulima kujiendeleza kibiashara.
Rwechungura ameongeza kuwa shirika lake pia litanunua mashine kwa ajili ya kusindika bidhaa hizo itakayogharimu jumla ya shilingi milioni kumi.

Ameongeza kuwa mradi wa EU KUWAKI umewezesha akina mama kujiunga katika vikundi mbalimbali na kuwawezesha kupata mikopo na mafunzo ya kusindika na kukausha mazao yao kutoka kwa shirika la viwanda vidogovidogo (SIDO) Mkoani Singida.

Rwechungura amesema katika kata ya Gumanga Vikundi vilivyoundwa ni kumi vyenye jumla ya wakulima 229 mabao mpaka sasa wana hisa zenye thamani ya shilingi milioni 26 na wameshatoa mikopo kwa wanakikundi 138 yenye thamani ya shilingi milioni 23.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew Mtigumwe akiangalia bidhaa zinazozalishwa na kikundi cha akina mama cha wakulima wa mbogamboga na matunda cha Gumanga Wilayani Mkalama.

Katika kikao cha wadau wa kilimo cha mboga mboga Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew Mtigumwe amewataka wadau hao kwa kushirikiana watafakari namana ya kutatua changamoto za wakulima hao.

Mtigume amesema wakulima wa mbogamboga na mattunda wanakabiliwa na changamoto ya kukosa maji ya uhakika kwa ajili ya umwagiliaji wa mazao hao, jambo alilolishuhudia alipotembelea mashamba yao.

Ameongeza kuwa changamooto nyingine ni ukosefu wa soko la uhakika  na kuwataka SIDO, Helvetas na wadau wengine kuwasaida wakulima hao katika kuwatafutia masoko.

Meneja wa Shirika la SIDO Mkoa wa Singida Shoma Kibende akchangia mada katika kikao cha wadau wa kilimo cha mbogamboga na matunda.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew Mtigumwe katika picha ya pamoja na waadau wa kilimo cha mbogamboga na matunda.

No comments:

Post a Comment