Monday, April 18, 2016

NAPE AUNGURUMA SINGIDA

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mheshimiwa Nape M. Nnauye ( Aliyesimama) akizungumza na wadau wa sekta za wizara yake kwa Mkoa wa Singida  katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa Singida katika kikao kilichofanyika jumamosi jioni.

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Singida, Ndugu Saidi Ali Amanzi akitoa taarifa ya Mkoa mara baada ya kuwasili kwa Mheshimiwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape M. Nnauye.

Kaimu Mkurugenzi wa kituo cha kurushia matangazo cha Televisheni ya taifa (TBC) Mkoa wa Singida, Israel Bunamba akisoma taarifa ya huduma za kituo hicho kwa Mkoa wa Singida kwa Mheshimiwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape M. Nnauye na wadau waliohudhuria kikao.
Mwakilishi wa Mamlaka ya Mawasiliano  Tanzania  (TCRA) Kanda ya Kati Mhandisi Ngeela akisoma taarifa ya Mamlaka hiyo kwa Mheshimiwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape M. Nnauye.
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Mary Maziku akizungumza machache katika kikao cha wadau wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo waliohudhuria kikao hicho.

Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo mheshimiwa Nape Moses Nnauye  jana alikutana na wadau wa sekta za wizara yake katika kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Singida.

Katika kikao hicho Nape alizungumzia kila sekta inayohusiana na wizara yake kwa kina ambapo kwa upande wa sekta ya habari msisitizo mkubwa ulikuwa ni halmashauri ambazo hazina maafisa habari  zitenge bajeti na kuajiri wataalam hao ili kutengeneza daraja kati ya vyombo vya habari na serikali.

Pia mheshimiwa Nape aliagiza na kusisitiza wakurugenzi wa halmashauri zote, wakuu wa idara na viongozi mbalimbali wa Wilaya wawaruhusu maafisa habari kuingia kwenye vikao vyote vya maamuzi ili waweze kuwa na  taarifa sahihi na za kutosha pindi wanapokutana na vyombo vya habari.

“Tanzania ina magazeti 15 yanayotoka kila siku na magazeti haya habari zake kubwa ni zile zinazohusiana na serikali, maafisa habari wasipoingia kwenye vikao vya maamuzi watawakimbia waandishi wa habari na waandishi wa habari wasipopata habari wanaenda kuandika habari za uongo au zisizo na ubora” Aliongeza Nape.

Akisisitiza juu ya hilo alisema kuna kipindi Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilikuwa kina sifa mbaya sana kwa jamii hivyo akawaomba viongozi wakuu wa chama awe anaingia kwenye vikao vyote vya maamuzi hata vile ambavyo vitashirikisha watu watatu tu.

“Baada ya kuanza kuingia kwenye vikao vya chama, kwanza mi nikawa ndo msemaji mkuu wa chama na nikaanza kutoa taarifa sahihi kwa waandishi wa habari katika kila kilichokuwa kinaendelea ndani ya chama,na hatimaye heshima na hadhi ya chama ikarejea” Alisema Nape.



Kwa upande wa Michezo alisisitiza kufanyika kwa mchakato wa kutafuta viongozi imara katika ngazi za Wilaya na mikoa ili kuepuka viongozi wanaowekwa na viongozi wakuu wa taifa kwa ajili ya kuwapigia kura tu kwenye vikao vya kamati kuu.

“Kuna sehemu nilienda nikauliza nyie kiongozi wenu nani, wakasema kuna bwana mmoja alikuja hapa akatupa pesa tukampigia kura akaondoka zake, Hiyo ni hatari sana na jambo hili ni lazima likomeshwe” Alisisitiza Nape.

Kwa upande wa Sanaa na utamaduni, Mheshimiwa Nape alisisitiza kujengwa kwa vituo vya maonesho ya kumbukumbu katika kila mkoa ili kurahisisha shughuli za utalii na kukuza uchumi wa mkoa husika.


“Hapa Singida kuna vivutio vingi sana vya utalii lakini hakuna sehemu maalum ambayo hata mtu akitaka kufahamu historia mbalimbali ya watu na vitu vya kale vilivyopo, ni lazima tuweke vituo ambavyo tutakusanya vivutio vyote vya mkoa na kuviweka sehemu moja” alimalizia Nape.
Source :- www.mkalamayetu.blogspot.com

No comments:

Post a Comment