Wednesday, June 01, 2016

WAKULIMA WA PAMBA KUSAIDIWA KUPATA SULUHISHO LA CHANGAMOTO YA VIUATILIFU VILIVYOSHINDWA KUFANYA KAZI

Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dokta Angelina Mageni Lutambi akizungumza na wadau wa zao la Pamba Mkoani Singida.

Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dokta Angelina M. Lutambi ameahidi kufuatilia na kuhakikisha suluhisho linapatikana kwa wakulima wa zao la Pamba waliopatiwa dawa za kuuwa wadudu waharibifu ambazo hazikufanya kazi  na kusababisha uharibifu mkubwa Mkoani Singida. 

Dokta Lutambi ameyasema hayo katika mkutano wa wadau wa zao la pamba uliofanyika Wilayani Manyoni ambapo wakulima wametoa malalamiko yao kuhusu dawa ya kuuwa wadudu aina ya Ninja kushindwa kuua wadudu waharibifu.

Ameongeza kuwa suala hilo atalifikisha katika Wizara ya Kilimo, chakula na ushirika ili kuona namna ya kuwasaidia wakulima hao ambao huendesha kilimo hicho kwa mkataba.

Aidha ameziagiza halmashauri zote za Wilaya Mkoani Singida kwa kushirikiana na bodi ya pamba na kampuni ya Biosustain inayoendesha kilimo hicho kwa Mkataba kufanya tathmini ya hasara iliyopatikana ili kufanya maamuzi sahihi.


Mkulima Timothy Nkulu kutoka kata ya Misughaa Wilayani Ikungi (aliyesimama).

Mkulima Timothy Nkulu kutoka kata ya Misughaa Wilayani Ikungi ameeleza kuwa alianzisha shamba darasa la zao la pamba la ukubwa wa ekari tatu ila amepata hasara kubwa kutokana na wadudu kushambulia zao hilo huku dawa ya kuuwa wadudu aina ya Ninja aliyopewa ikishindwa kufanya kazi.

Nkulu ameongeza kuwa alifanya kazi kubwa ya kuwahamasisha wakulima wenzake kulima zao hilo ila kutokana na hasara aliyoipata wakulima wenzake wamekata tamaa ya kulima tena zao hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Christopher Ngubiagai akichangia hoja katika kikao cha wadau wa Pamba.

No comments:

Post a Comment