Monday, May 30, 2016

MKUU WA MKOA AAPA KUSIMAMIA FEDHA ZA KAMPENI YA KITAIFA YA USAFI WA MAZINGIRA

 Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew J. Mtigumwe. 

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew J. Mtigumwe ameapa kusimamia fedha za kampeni ya kitaifa ya usafi wa mazingira Mkoani Singida.

Mhandisi Mtigumwe ameyasema hayo katika kikao cha kutathmini utekelezaji wa kampeni hiyo huku akieleza kuwa katika kipindi cha mwaka 2015/2016 serikali ilitoa shilingi milioni 417 kwa ajili ya ujenzi wa vyoo bora na vifaa vya kunawia elfu 55.

Amesema kuwa ni jambo la aibu kwa mwananchi kukosa choo huku akiwasisitiza watendaji kuendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa vyoo bora  na madhara ya  kutokuwa na mazingira safi  kwani hupelekea magonjwa ya mlipuko.

Pia Mhandisi Mtigumwe amewaagiza wakurugenzi kusimamia usafi wa mazingira hadi ngazi ya chini, kuanzisha na kusimamia sheria ndogondogo pamoja kuweka adhabu kali kwa watakaokiuka sheria hizo.

Naye Mratibu wa Kampeni ya Usafi wa Mazingira Mkoani Singida Habibu Said Mwinory amesema watahakikisha kuwa wanafanya ukaguzi wa maeneo yote na kutoa elimu ya usafi wa mazingira ili kujihakikishia Mkoa unakuwa katika hali ya usafi.

Mwinory amesema wiki ya kwanza ya kila mwezi watakuwa wakikagua maeneo yote ya biashara kama nyumba za kulala wageni, baa na hoteli, wiki ya pili ukaguzi utakuwa katika taasisi mbalimbali kama vile ofisi, shule na vyuo wakati wiki ya tatu na nne ukaguzi utakuwa katika maeneno ya makazi.

Ameongeza kuwa zoezi hilo litakuwa endelevu na kuwataka wananchi wote kufanya usafi na sio kusubiri mpaka wakaguliwe au wachukuliwe hatua kwa kushindwa kuifanya hivyo.

No comments:

Post a Comment