Tuesday, November 04, 2014

MKUU WA MKOA AWATAKA WATUMISHI WAPYA KUFANYA KAZI KWA BIDII.


Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Parseko Vicent Kone.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Parseko Vicent Kone amewataka watumishi wapya  na wale waliohamia katika Mkoa wa Singida kufanya kazi kwa bidii kwani hawajahamia Mkoa huu kuziba nafasi za kazi bali kufanya kazi.

Dokta Kone ameyasema hayo leo asubuhi wakati akifungua kikao cha Kamati ya Kusimamia, Kudhibiti na Kuratibu matumizi ya Sekretarieti ya Mkoa, ambacho kimefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Amesema mtumishi yeyote aliyehamia Mkoa wa Singida kwa dhana ya kutegea kazi basi hafai kubaki katika mkoa huu na ametoa ruhusa atafute mkoa mwingine kwakuwa sifa ya watumishi wa mkoa huu ni utendaji mzuri wa kazi.

Dokta Kone ameongeza kuwa watumishi wanaopenda kukaa ofisini kusubiri muda wa kazi uishe hawataki katika ofisi yake bali watumishi waadilifu na wachapakazi ndio wanaopaswa kubaki katika Mkoa wake.

Amesema ongezeko la watumishi katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa lilete tija katika kuongeza utendaji kazi na kutimiza majukumu ya  Sekretarieti ya Mkoa na kusisitiza matumizi mazuri ya muda wa kazi hasa kutokutumia muda mwingi katika vikao.


 Katibu Tawala Mkoa wa Singida Liana A. Hassan.

No comments:

Post a Comment