Wednesday, October 29, 2014

RAIS WA ZAMBIA MICHAEL SATA AFARIKI DUNIA.




Michael Sata, Rais wa Zambia.

Baada ya siku ya Jumanne kuamkia Jumatano kuzagaa kwa uvumi kuhusu kufariki kwa rais wa Zambia Michael Sata, hatimaye hii leo Serikali ya nchi hiyo imethibitisha kifo chake.

Sata aliyekuwa na umri wa miaka 77 alisafiri kuelekea jijini London Uingereza juma moja lililopita kwa ajii ya kupata matibabu zaidi lakini hii leo katibu wa baraza la Mawaziri, Roland Msiska amethibitisha kifo chake.

Akitoa tangazo hilo mapema leo alfajiri, Roland amewaambia wananchi wa Zambia kwa masikitiko makubwa angependa kutangaza kifo cha rais wao aliyekuwa akipatiwa matibabu nchini Uingereza.

Tangazo hili linathibitisha madai ya vyama vya upinzani na watu wa karibu wa rais Sata ambao mara kadhaa walidai kuwa kiongozi huyo anaugua na ameshindwa kutekeleza majukumu yake kama rais lakini mara zote Serikali imekuwa ikikanusha hadi juma moja lililopita ilipothibitisha kuugua kwa rais Sata.

Wakati alipokuwa akiondoka kuelekea jijini London kwa matibabu, rais Sata alimteua waziri wa ulinzi na sheria Edgar Lungu kukaimu madaraka ya rais kwa kipindi ambacho hatokuwepo.

Makamu wa rais Guy Scott ambaye mara kadhaa amekuwa akishiriki shughuli mbalimbali za Serikali kama kiongozi wa nchi, yeye ana uraia wa Uskochi hali ambayo inamfanya ashindwe kuwa rais kamili wa taifa la Zambia kwakuwa wazazi wake hawakuzaliwa nchini Zambia.
 
Michael Sata, Rais wa Zambia.

Sata ambaye alibatizwa jina la "King Cobra" na wafuasi wake wakati alipochaguliwa mwaka 2011, alionekana kama mbadala wa siasa za Zambia na mtu ambaye alikuwa wa vitendo licha ya kukosolewa kwa sehemu kubwa na upinzani.

Hivi karibuni rais Sata alianza operesheni dhidi ya wapinzani wake na waandishi wa habari waliokuwa wakikosoa Serikali yake jambo ambalo lilianza kumchora kama mmoja wa viongozi wababe kusini mwa bara la Afrika.

Picha na taarifa kwa hisani ya tovuti ya RFI kiswahili.

No comments:

Post a Comment