Monday, March 24, 2014

UFUNGUZI WA KITUO CHA KUTOA HUDUMA KWA WATOTO WALIO KATIKA MAZINGIRA HATARISHI "SAYUNI CENTRE" TAREHE 22-3-2014 MANYONI MJINI


Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Parseko Vicent Kone amezindua kituo cha kutoa huduma kwa watoto walio katika mazingira hatarishi kinachoitwa Sayuni kilichopo wilaya ya Manyoni, Mkoani hapa.

Katika uzinduzi huo Dkt. Kone amelishukuru shirika la Outreach International kwa ujenzi wa kituo hicho pamoja na misaada ya chakula na huduma za afya zinazotolewa na shirika hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Parseko Vicent Kone akizindua kituo cha kutoa huduma kwa watoto walio katika mazingira hatarishi cha Sayuni Wilayani Manyoni, Kushoto kwake ni Kathy Hamilton na aliyeinama ni Rais wa Outreach International Floyd Hammer.  

Dkt. Kone amesema Rais wa Outreach International Floyd Hammer na mkewe Kathy Hamilton ni watu wenye upendo kwani wamejitolea kusaidia watoto hao nchini Tanzania hasa katika Mkoa wa Singida kwa kujenga vituo hivyo na kutoa misaada mingine.

Amesema Floyd na Mkewe Kathy si matajiri sana lakini wameweza kujenga vituo viwili, cha kwanza kikiwa ni Singida Children and Community Centre kilichopo mjini Singida pamoja na hiki kilichozinduliwa cha Sayuni Centre.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Parseko Vicent Kone (katikati), Kushoto kwake ni Kathy Hamilton na kulia ni Rais wa Outreach International Floyd Hammer wakifurahia sherehe za  uzinduzi wa kituo cha kutoa huduma kwa watoto walio katika mazingira hatarishi cha Sayuni Wilayani Manyoni
 Baadhi ya wanafunzi wakifurahia sherehe za  uzinduzi wa kituo cha kutoa huduma kwa watoto walio katika mazingira hatarishi cha Sayuni Wilayani Manyoni

Dkt. Kone amesema watoto wanaopatiwa Chakula katika kituo cha Singida waliofanya mtihani wa Darasa la Saba mwaka huu wote wamefaulu kujiunga na kidato cha Kwanza kwa mwaka huu hii ikiwa ni ishara ya kufanikiwa kwa kituo hicho.

Kwa upande wake Raisi wa Outreach International Floyd Hammer na mkewe Kathy Hamilton wamemshukuru Dkt. Kone  na Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Fatma Toufiq kwa ushirikiano wao katika ujenzi wa kituo hicho.

Aidha, Makamu wa Rais wa Outreach International Tanzania Dkt. Michael Wilhelm Kitwaka amesema ujenzi wa kituo cha Sayuni ulianza rasmi Aprili, 2013 na umegharimu kiasi cha shilingi za kitanzania milioni 240.

Dkt. Kitwaka amesema kituo hicho ambacho ni kikubwa kwa Mkoa wa Singida na cha pili kujengwa kitatoa huduma  kwa watoto watakaokubali kuingia darasani na kusoma.


Amesema Kituo hicho kinatarajia kuhudumia watoto 100 na kitasaidia kuongeza kiwango cha ufaulu kwa watoto hao huku kikipunguza idadi ya watoto wanaoacha shule kwa kukosa mahitaji maalumu kama chakula.


 Makamu wa Rais wa Outreach International Tanzania Dkt. Michael Wilhelm Kitwaka.

Katika Sherehe hizo baadhi ya viongozi wamepanda miti katika eneo la kituo cha kutoa huduma kwa watoto walio katika mazingira hatarishi cha Sayuni kilichopo wilaya ya Manyoni, wakitanguliwa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Parseko Vicent Kone.


Rais wa Outreach International Floyd Hammer na mkewe Kathy Hamilton nao wamepanda mti;

Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Fatma Hassan Toufiq na Mkuu wa Msafara wa Madaktari kutoka Marekani Deborah Turner wamepanda mti kwa pamoja katika eneo hilo.

Moja ya shughuli walizozifanya madaktari kutoka marekani waliojitolea ni kutoa huduma kwa watoto wenye matatizo mbalimbali.
Hawa ni baadhi ya watoto waliohudumiwa na madaktari hao. 

No comments:

Post a Comment