Friday, March 21, 2014

BALOZI WA JAMHURI YA WATU WA NCHINA TANZANIA ATEMBELEA MKOANI SINGIDA

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Parseko V. Kone ametembelewa na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania Mhe. Dkt Lu Youqing jana asubuhi ofisini kwake.
 
Balozi Youqing  amefanya ziara mkoani Singida ili kujadili mipango ya sasa na ya baadaye ya kimaendeleo Mkoani Singida ili kuona maeneo ya uwekezaji ambayo yatainua pato la mwananchi.

Katika ziara hiyo Balozi Youqing ameambatana na Mwakilishi Mkuu wa Uwakilishi wa Kiuchumi na Kibiashara wa Jamhuri ya Watu wa China Nchini Bw. Lin Zhiyong pamoja na Afisa wa Ubalozi huo Bw. Ren Zhihong.


Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Parseko V. Kone (katikati) akiwa na  Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania Mhe. Dkt Lu Youqing (wa kwanza kushoto), anayefuata ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, SACP Geofrey Kamwela, wa kwanza kulia ni Mwakilishi Mkuu wa Uwakilishi wa Kiuchumi na Kibiashara wa Jamhuri ya Watu wa China Nchini Bw. Lin Zhiyong akifuatiwa na Katibu Tawala Mkoa wa Singida Liana Hassan, Nyuma yake ni Katibu wa Mkuu wa Mkoa Hussein Mwatawala.

Amesema wawekezaji kutoka China wako tayari kuwekeza Mkoani Singinda na tayari kampuni moja kutoka China imeonyesha nia ya kutaka kuwekeza katika umeme wa kutumia nishati ya upepo.

Balozi Youqing  ameongeza kuwa Tanzania ina hitaji umeme wa uhakika na wenye gharama ambazo wananchi watazimudu, akisisitizia umeme wa upepo ambao amesema hauchafui mazingira.

Ameongeza kuwa wawekezaji kutoka China wanaweza kuwekeza kwenye kilimo na ufugaji Mkoani Singida ili kukuza uchumi wa mwana Singida.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Parseko V. Kone  akiwa na  Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania Mhe. Dkt Lu Youqing (wa kwanza kulia), anayefuata ni Mwakilishi Mkuu wa Uwakilishi wa Kiuchumi na Kibiashara wa Jamhuri ya Watu wa China Nchini Bw. Lin Zhiyong.
Balozi Youqing  amesisitiza kuwa kutokana na historia ya ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na China, kwa sasa Sekretarieti za Mikoa na Serikali za Mitaa zina fursa ya kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mikoa nchini China ili kujifunza teknolojia mbalimbali, kutafuta kampuni za uwekezaji  na kubadilishana uzoefu katika maeneo mbalimbali.
Ameongeza kuwa ameona jitihada za dhati zinazofanywa na Mkuu wa Mkoa katika kuleta maendeleo kupitia kilimo na ufugaji Mkoani Singida.
Kwa upande wake Dkt. Kone amemshukuru Balozi Youqing kwa kuonyesha nia ya kushirikiana naye katika kuleta maendeleo ya Mkoa wa Singida hasa katika kusaidia kupata wawekezaji katika mradi wa umeme wa nishati ya upepo.
Dkt. Kone amesema mradi wa umeme wa upepo hautaunufaisha Mkoa wa Singida peke yake bali taifa kwa ujumla kwa kutoa fursa za ajira, ongezeko la viwanda  na umeme wa uhakika.
Ameongeza kuwa wawekezaji kutoka China wana fursa mbalimbali za uwekezaji Mkoani Singida kama vile kilimo na ufugaji, akitilia mkazo uwekezaji katika mazao ya alizeti, vitunguu, pamba na mpunga.
Dkt. Kone amesema wananchi wa Singida wanafuga Kuku bora wa asili ambapo uwekezaji ukifanyika utawaongezea kipato.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Parseko V. Kone  akiwa na  Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania Mhe. Dkt Lu Youqing (wa kwanza kulia), anayefuata ni Mwakilishi Mkuu wa Uwakilishi wa Kiuchumi na Kibiashara wa Jamhuri ya Watu wa China Nchini Bw. Lin Zhiyong.
Aidha Mkoa wa Singida unatoa asali bora nchini hivyo uwekezaji  katika sekta ya ufugaji nyuki na kiwanda cha kuchakata asali na nta utaongeza thamani ya mazao hiyo.
Balozi Youqing amekuwa balozi wa kwanza kuutembelea Mkoa wa Singida kwa Mwaka 2014. Mkoa wa Singida umewahi kutembelewa na Mabalozi kutoka Ireland, Marekani, Kenya, Nigeria na Uingereza.

No comments:

Post a Comment