
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Mhe. Suleiman Yusuph Mwenda, amefunga kongamano la maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi yaliyofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego, na kusisitiza kuwa elimu ndiyo msingi wa kuondoa ujinga na kuimarisha maendeleo ya Taifa.
Akihutubia wadau wa elimu, Wanafunzi na wananchi waliohudhuria maadhimisho hayo, Mhe. Mwenda amesema wiki ya elimu ya watu wazima inalenga kuhamasisha kila mwanadamu atambue haki yake ya kupata elimu.
“Elimu ya watu wazima ni muhimu sana kwa kupata ujuzi unaomwezesha mtu kujiajiri. Pia inamuondoa mtu kwenye ujinga na kumwezesha kuendana na zama za sasa za kidigitali kupitia sayansi na teknolojia,” amesema.
Aidha ameongeza kuwa Mkoa wa Singida umeendelea kupiga hatua kubwa kielimu kuanzia shule za awali hadi vyuo vikuu, na matokeo yake ni ufaulu mkubwa wa vijana. “Vijana wetu wanafaulu kwa asilimia 98, jambo linaloonesha mabadiliko makubwa ukilinganisha na miaka iliyopita. Hii inatupa matumaini makubwa ya mustakabali wa elimu,” ameongeza.
Mhe. Mwenda amesisitiza kuwa serikali inaendelea kuwekeza kwenye miundombinu na vifaa vya kufundishia ili kuhakikisha fursa za elimu zinapatikana kwa wote.
“Shule mpya zimejengwa na zinaendelea kujengwa ili vijana wetu wasome hadi kidato cha tano na sita na hatimaye vyuo vikuu,” amesema.
Akisoma ripoti ya Hali ya elimu ya Watu wazima katika Mkoa wa Singida, Afisa Elimu ya Watu Wazima Mkoa wa Singida, Bi. Sarah Mkumbo, ameeleza kuwa mkoa wa Singida una jumla ya shule za msingi 691 na sekondari 194, zote zikitumika pia kama vituo vya elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi. Amesema pia Singida inayo vyuo mbalimbali vikiwemo vya walimu, afya, maendeleo ya jamii, VETA na Chuo Kikuu Huria.
Bi. Mkumbo ameongeza kuwa mkoa unatekeleza programu kadhaa ikiwemo MUKEJA yenye zaidi ya wanafunzi 111,000 wanaojifunza masomo yenye manufaa, pamoja na wengine zaidi ya 136,000 wanaoshiriki kwenye elimu ya uzalishaji mali. “Programu hizi zimekuwa kichocheo cha kupunguza ujinga na kuongeza maarifa ya vitendo miongoni mwa wananchi,” amesema.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Mhe. Moses Machali, amesema elimu ni kila kitu katika msingi wa maendeleo ya jamii. “Shule nyingi zinahitaji kuja kujifunza Singida kwa sababu elimu yetu inajikita kwenye vitendo. Hii imekuwa msaada mkubwa katika kuibadilisha jamii nzima,” amesema.
Mhe. Machali ameongeza kuwa kila jamii iliyofanikiwa duniani imepiga hatua kupitia elimu. “Vijana hawa wanapaswa kuwezeshwa ili waweze kuibadilisha jamii. Mambo yote duniani—iwe ni afya, biashara au teknolojia—yanahitaji elimu ili kufanikishwa kwa ufanisi,” amesema.
Maadhimisho hayo yamehitimishwa kwa msisitizo kwamba elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi si chaguo bali ni hitaji la lazima katika zama za kidigitali, ili kujenga taifa linalojitegemea, lenye mshikamano na maendeleo endelevu.Tukio hilo limebeba kaulimbiu isemayo “Kukuza kisomo katika zama za kidigitali kwa maendeleo endelevu ya taifa letu.”
Kutazama yaliyojiri katika maadhimisho hayo fungua kiungo kilichopo hapo chini: