Wednesday, March 06, 2024

KILA KIJIJI KUCHIMBIWA KISIMA CHA MAJI SAFI MKOANI SINGIDA

 

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba, leo tarehe 6 Machi, 2024 amefanya ziara ya kukagua utekelezaji wa ujenzi wa Miradi ya Maji inayotekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini katika Wilaya ya Mkalama na Iramba mkoani humo. Akizungumza katika nyakati tofauti Serukamba amemuagia Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini Mkoa wa Singida Mhandisi Lucas Said, kuhakikisha kila kijiji mkoani humo ambacho kinachangamoto ya upatikanaji wa maji kinachimbiwa kisima pamoja na kujengewa miundombinu imara ili wananchi waweze kupata maji kwa ukaribu kwa kuwa gari la kuchimba lipo. "Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameshatuletea gari la kuchimbia visima, sasa siona sababu ya wananchi kukosa huduma ya maji, natoa wiki mbili kila halmashauri iniletee mpango kazi wake kuhusu utekelezaji wa huduma ya maji vijijini" RC Serukamba

Aidha Mkuu wa Mkoa huyo ametoa rai kwa wananchi hususani jumuiya ya watumia maji kutunza miundombinu ya maji iliyojengwa na inayotekelezwa katika maeneo yao kwa kutokata mabombo, kulinda vyanzo kwa kupanda miti pamoja na kutumia maji vizuri. "Serikali imetuletea huduma ya maji safi na salama, hizi ni juhudi za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali wananchi wake, ninawaomba tumuunge mkono kwa kuitunza miradi hii ili itutunze" RC Serukamba Naye Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini Mkoa wa Singida Mhandisi Lucas Said, amemhakikisha Mkuu wa Mkoa huo kwamba kuanzia mwezi huu Machi, gari hilo litakuwa na ratiba ya kuchimba visama vya maji kwenye maeneo ambayo yanachangamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo.

Akitoa taarifa ya hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika Wilaya ya Mkalama Kaimu Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mhandisi Omary Matembo, amesema kwa sasa ni asilimia 68.23 sawa na wananchi 174,346 wanaopata huduma hiyo kati ya wananchi wote 255,514.

Mhandisi Matembo, amefafanua kuwa huduma ya maji katika Halmashauri ya Wilaya hiyo hutokana na vyanzo vya maji chini ya ardhi ambavyo ni visima virefu, vifupi na vya kati ambapo katika miundombinu ya maji iliyopo vituo vya kuchotea maji (water points) ikiwa ni jumla ya 885.

Naye Meneja wa RUWASA Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Mhandisi Ezra J. M, amesema ujenzi wa mradi wa maji kwa vijiji vya Galangala na Kisharita vilivyopo kata ya Kinampanda umeanza tarehe 2 Oktoba, 2023 na unatarajiwa kukamilika tarehe 2 Aprili, 2024 ambapo gharama ya mradi ni Shilingi 976,636,255.04 na utekelezaji kwa sasa umefikia asilimia 85 na ukikamilika utawanufaisha zaidi ya watu 8,782.

Kwaupande wao wananchi wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwasogezea huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa vijijini na kueleza kuwa huduma hiyo imeongeza hali ya kiuchumi, kifamilia kwakuwa imepunguza muda mwingi uliokuwa ukitumika kwaajili ya utafutaji maji sambamba na kuepushwa na magonjwa yatokanayo na maji machafu.





No comments:

Post a Comment