Monday, February 26, 2024

RC SINGIDA AAGIZA TARURA KUSIMAMIA UJENZI DARAJA LA MINYUGHE LIKAMILIKE HARAKA

MKUU wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba ameiagiza Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) mkoani hapa kusimamia ujenzi wa daraja la Minyughe lililopo Wilayani Ikungi linalojengwa na kampuni ya JP Traders Limited ili liweze kukamilika haraka na wananchi waanze kusafiri kutoka upande wa kata ya Minyughe kwenda upande wa kata ya Makilawa.

Serukamba ametoa agizo hilo jana (Februari 26, 2024) alipotembelea daraja hilo ambalo lilikatika tangu Oktoba mwaka jana kulikagua kuangalia maendeleo ya ujenzi wake ikiwa ni mfululizo wa ziara yake ya kukagua miradi ya ujenzi na matengenezo ya barabara, madaraja na vivuko  katika Wilaya zote za mkoani hapa.

Alisema pia daraja hilo litakapokamilika TARURA ihakikishe barabara inachongwa vizuri ili iweze kupitika muda wote na katika bajeti ijayo ifikirie namna ya kulinda Mto Saiwa ili usiweze kuathiri daraja baadaye hasa kutokana na mwenendo wake wa kupanuka kila mara.

“Mto huu unasogea kila wakati na kupanuka, hivyo tusipofanya jitihada za kuulinda itafika wakati daraja litaelea pekee yake na kuhatarisha hatimaye likabomoka wakati limejengwa kwa gharama kubwa,”alisema RC Serukamba.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akizungumza na baadhi ya wananchi wa waliojitokeza watika wa ziara ya Mkuu wa mkoa huyo alipotembelea kukagua ujenzi wa daraja la Minyughe lililopo Wilayani Ikungi tarehe 26 Februari, 2024.

“Utaona gharama za ujenzi wa daraja hili ni takribani Sh.bilioni mbili ambalo linahudumia kata tatu tu pesa kama hizi pengine zingeweza kutumika kujenga barabara za kuunganisha Wilaya kwa Wilaya au Mkoa kwa Mkoa lakini Rais wetu Samia Suluhu Hassan ameona angalau kila kijiji kwa kijiji kiweze kupitika, wananchi tumshukru sana Rais huyu wa awamu ya Sita.” alisisitiza.

Aidha, Mkuu wa Mkoa aliwataka wananchi kuongeza juhudi katika kilimo kwani daraja na barabara itakuwepo kwa ajili ya kuwarahisishia kusafirisha mazao yao kwa ajili ya kuyapeleka kwenye masoko kwaajili ya biashara mbalimbali zikiwemo za mazao ya biashara.

Hata hivyo aliwasihi wananchi wabadilike katika kilimo kwa kuhakikisha wanaongeza matumizi ya mbolea ili kuongeza uzalishaji wa mazao wenye tija kwao na halmashauri husika.

“Wanasayansi wanasema ekari moja ya mahindi ukiweka mifuko mitano miwili ya kupandia, mitatu ya kukuzia unapata maguni 30 hadi 35 kwa ekari moja lakini leo nyie mkipata zaidi ni maguni mawili au matatu, lazima tutoke huko na namna ya kutoka ni kuongeza matumizi ya mbolea,”alisema Serukamba.

Meneja wa TARURA Mkoa wa Singida, Mhandisi Ibrahimu Kibasa akitoa taarifa ya mradi wa ujenzi wa daraja la Minyughe kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba mara baada ya kuwasili kukagua ujenzi wa daraja hilo Wilayani Ikungi tarehe 26 Februari, 2024.

Awali Meneja wa TARURA Mkoa wa Singida, Mhandisi Ibrahimu Kibasa, alimweleza Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba, kuwa daraja hilo limeanza kujengwa na utekelezaji wake umefikia asilimia 60 na linatakiwa kukamilika Mei 18, 2024.

Alisema hadi sasa kazi zilizofanyika ni kutengeneza njia ya mchepuko, kupanga mawe na kusuka nondo, kumwaga zege la chini na la juu na ulindaji wa daraja kwa kutumia mawe ambapo Mkandarasi wa kampuni ya Mzava M/S JP Traders Limited aliyepewa kazi hiyo kwa kulijenga kwa Sh, Milioni 556.140, hadi sasa ameshalipwa Sh. Milioni 224.770 sawa na asilimia 40.4 ya thamani ya mkataba wote.

“Barabara ya Mtamaa - Minyughe hadi Mtavira ambayo daraja hili lipo ni la muhimu sana kwa wananchi wa kata za Minyughe na Makilawa kwani maji yakijaa katika daraja wanafunzi wanashindwa kwenda shule au wananchi kushindwa kufuata huduma za matibabu.” alisema.

Kibasa alitoa mchanganuo kuwa gharama za kununua vyuma vitakavyowekwa juu ya daraja hilo vinagharimu Sh.milioni 939 hivyo jumla ya mradi ni Sh.bilioni 1.4 ambapo zikijumlishwa gharama za kodi bandarini na usafirishaji kutoka Dar es Salaam kuja Singida gharama zote za mradi zitafikia takribani Sh.bilioni 2 kasoro.

MATUKIO KATIKA PICHA WAKATI WA ZIARA YA UKAGUZI WA UJENZI WA DARAJA

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akizungumza na Waandishi wa habari mara baada ya ukaguzi wa daraja la Minyughe lililopo Wilayani Ikungi tarehe 26 Februari, 2024.


Muonekano wa sehemu ya ujenzi wa daraja hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akisisitiza jambo wakati wa ziara hiyo.



Baadhi ya wananchi wakizungumza na kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa daraja hilo ambapo wamesema linaenda kuondoa adha ya usafiri na usafirishaji waliyokuwa wakiipata kwa muda mrefu.

No comments:

Post a Comment