Thursday, November 02, 2023

MGOGORO WA WAKULIMA NA WAFUGAJI ULIODUMU ZAIDI YA MIAKA 12 ITIGI WAISHIA MIKONONI MWA SERUKAMBA

MKUU wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, ametatua mgogoro  wa Wafugaji na Wakulima wa Vijiji vitatu vilivyopo katika Halmashauri ya Itigi Wilayani Manyoni uliodumu kwa zaidi ya miaka 12 hadi sasa kwa kuamuru kila Kijiji kipange matumizi bora ardhi na kuwekewa mipaka.

Eneo lililokuwa likigombaniwa na Wakulima na Wafugaji lipo katika Kijiji cha Doloto ambalo vijiji vitatu vya Dang'welu, Itigi na Doloto vimelizungu ambapo kila kijiji kinadai eneo hilo ni lake.

Akizungumza na Wananchi wa vijiji vya Doloto, Dang'welu na Itigi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Doloto akiwa ameambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, alisema kuanzia sasa kila kijiji kipange eneo la malisho, kilimo na la kujenga makazi kulingana na mipaka iliyopo ya kila kijiji.

Serukamba alimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Itigi, John Mgalula ndani ya wiki mbili asimanie kila kijiji kitengeneze mpango wake wa eneo lake kwa kuweka eneo la malisho na kilimo na kuwekewa mpaka na kulitangaza  kwenye mkutano wa kila kijiji na Kamishna wa Ardi na Mpimaji wasimamie suala hilo na kutoa hati miliki ya ardhi.

"Kila kijiji kipange maeneo yake ya malisho yajulikane yawekewe mipaka na Kamishna wa Ardhi alitengenezee hati miliki la eneo hilo, naombeni ndugu sisi wote ni Watanzania Mungu ametusaidia tumekutana hapa Itigi na vijiji vyetu vimepakana tuheshimu mipaka ya kila kijiji," alisema

Serukamba alisema Serikali inawahitaji wakulima na wafugaji hivyo hakuna sababu ya kugombana na kwamba kama Kijiji kitatenga eneo dogo la kufuga halafu kikawa na mifugo mingi watambue kuwa watalazimika kuuza mifugo kuipunguza kwasababu haitaruhusiwa kwenda kulisha mifugo kwenye eneo la kijiji kingine.

"Tumeamua hivyo sababu umoja umewashinda sasa sisi hatutaki migogoro kwenye nchi yetu, nchi inaongozwa kwa sheria lakini pia ipo sheria ya ardhi na sheria ya kuanzishwa vijiji ambazo zinapaswa kuheshimiwa na msizuie mtu akipita na ng'ombe eneo kwenda mfano mnadani," alisema.

Serukamba alisema kila mtu akae kwenye Kijiji chake na kama ikitokea mtu anataka kuhamia kwenye kijiji kingine na  akapokelewa ni sawa lakini haiwezekani mtu aishi kijiji cha Doloto halafu akachungie mifugo kijiji cha Dang'welu.

Naye Mkazi wa Kijiji cha Doloto, Khamis Sungu alisema eneo la ardhi la kijiji hicho limekuwa na mwingiliano na vijiji vya Dang'welu, Itigi na Doloto ambapo lilivamiwa na wananchi kutoka vijiji vingine na hivyo wenyeji ambao ni wakazi wa Doloto wakakosa maeneo ya kulima na malisho.















No comments:

Post a Comment