Tuesday, October 31, 2023

KAMPENI YA JIKUBALI YAZINDULIWA RASMI MKOANI SINGIDA, SERUKAMBA ATOA ONYO KWA WANAUME WENYE TABIA YA KURUBUNI MABINTI

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba, amezindua Kampeni ya JIKUBALI Kimkoa kama ishara ya kuanza rasmi kwa jukwaa hilo Mkoani humo ili kutumika kutoa elimu na hamasa kwa wanafunzi wa rika balehe wanaosoma shule za Sekondari na jamii kuhusu mabadiliko ya tabia, kuwawezesha kuelewa masuala mbalimbali ya VVU na UKIMWI na namna ya kujikinga.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliyofanyika leo tarehe 31 Oktoba, 2023 katika Uwanja wa Bombadier uliyopo katika Manispaa ya Singida, Serukamba ametoa onyo kwa wanaume wenye tabia za kuwarubuni mabinti na wale wasiosikia mkono wa sheria utawafikia.

Aidha, amesema kampeni hiyo itawasaidia Wanafunzi kufahamu huduma zitolewazo kwa watu wenye maambukizi ya VVU pamoja na kuwajengea uelewa kuhusu masuala ya Afya ya uzazi.

Amesema, Vijana watawezeshwa jinsi ya kujiepusha na vishawishi vinavyoweza kuwafanya wasiyape kipaumbele masuala ya ngono mapema sambamba na mimba za utotoni pamoja na magonjwa ya ngono ikiwemo maambukizi ya VVU.

Kampeni hiyo inaenda sambamba na jitihada za nchi yetu katika kufikia malengo ya Kidunia ya TISINI NA TANO TATU ambayo tuliyaridhia mwaka 2015.  Malengo ya TISINI NA TANO TATU yana matarajio ya kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2025, asilimia 95 ya watu wanaoishi na VVU wawe wamepimwa na kujua hali zao za maambukizi ya VVU, asilimia 95 ya wanaojua hali zao wawe wanatumia dawa za kufubaza VVU, na asilimia 95 ya wanaotumia dawa wawe wamefubaza VVU katika miili yao”. Serukamba

Akizungumzia makundi yaliyolengwa amesema kuwa sababu za kuyalenga makundi hayo ya vijana katika kampeni hii ni kwasababu makundi yaliyo nyuma katika kufikia malengo ya TISINI NA TANO TATU ni kundi la VIJANA.

Amefafanua kwamba, vijana wengi wenye umri wa miaka 15 hadi 24 hawajui hali zao za maambukizi ukilinganisha na watu wenye umri mkubwa.

“Hivyo natoa wito kwa vijana na wasichana wa Mkoa wa singida kujitambua na kuchukua hatua kwa kujali kesho yao na kushinda vishawishi katika umri mdogo kama vile vizawadi, lifti za magari, bajaji, bodaboda, na hata baiskeli kutoka kwa watu usiowajua au ambao hawakutoa taarifa kwa wazazi au walezi”. Amesisitiza Serukamba 

Hata hivyo amewasihi Wazazi, Walimu na Watoa huduma za afya wa ngazi zote katika Mkoa wa Singida, kutimiza wajibu wao na kuzungumza na vijana, kutoa  huduma rafiki na  kujenga utamaduni wa kuwa karibu nao. Waalimu kuweka msisitizo wa ziada katika kutoa elimu ya afya shuleni na kuwasaidia watoto wanaoishi na maambukizi ya VVU bila ya kuwanyanyapaa.

Mkuu huyo wa Mkoa amesema Tanzania chini ya Uongozi Mahiri wa Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa kati ya nchi zinazoonesha mafanikio katika kupambana na maambukizi ya VVU kwa kiwango kikubwa.

Amesema, Mathalani katika Mkoa wa Singida kuongezeka kwa maeneo ya kutolea huduma za ushauri nasaha na upimaji wa VVU na Huduma rafiki za Vijana kutokana na Ujenzi wa Vituo vya kutolea Huduma za Afya hili ni moja ya mambo ambayo Serikali imeyafanya na kuongeza idadi ya watu wanaotambua hali zao na upatikanaji wa huduma rafiki kwa Vijana.

“Nitoe rai kwa vijana wote wajitokeze kwa wingi katika huduma za upimaji wa VVU kwa hiari ili wale watakaogundilika kuwa wana maambukizi ya VVU waweze kuanza dawa za ARV mapema ili watimize ndoto zao”. Serukamba

Serikali imepitisha sheria ya upimaji VVU ambayo imepunguza umri wa vijana wanaotakiwa kupima VVU kwa ridhaa ya mzazi au mlezi kutoka miaka 18 hadi 15, na pia kuruhusu huduma za upimaji binafsi wa VVU, ikiwa ni jitahada za kuwawezesha kutambua hali zao za maambukizi na kuchukua hatua stahiki za kujilinda.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Singida Fatuma Mganga, amesema Wazazi wanalo jukumu la kuwalea vijana hao ili kuwa na Taifa bora na lenye wafanyakazi hodari kwa maslai mapana ya familia na nchi kwa ujumla.

Aidha amewataka vijana kuacha tabia ya kuiga kila jambo, kujiepusha kuangalia picha zisizo na maadili katika mitandao ya kijamii pamoja na masuala ya ngono katika umri mdogo ili kufikia malengo waliyoyakusudia.

Hata hivyo amewahamasisha vijana Mkoani humo wa Kike na wa kiume walioko mashuleni wajitokeze kwa wingi kwenye kampeni hiyo ili kupata elimu na huduma mbalimbali zitakazotolewa.

Kampeni ya Jikubali inafanyika kwenye Mkoa wa Singida katika Wilaya ya Singida na katika Halmashauri ya Wilaya ya Iramba ambapo Wilaya nyingine za Manyoni, Ikungi, na Mkalama zitafikiwa na ujumbe kwa njia za vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

“JIKUBALI SHINDA VISHAWISHI KUWA BORA”

Katibu Tawala Mkoa wa Singida akisisitiza jambo wakati wa uzinduzi huo.









No comments:

Post a Comment