Wednesday, October 25, 2023

WANANCHI KIJIJI CHA SAGARA WAMPA MAUA RAIS SAMIA BAADA YA KUJENGEWA ZAHANATI

WAKAZI wa Kijiji cha Sagara Kata ya Itaja Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Mkoani Singida wamefurahishwa na ujenzi wa Zahanati ya Sagara iliyozinduliwa rasmi Oktoba 25, 2023 na Mkuu wa Mkoa huo Peter Serukamba ambapo wamemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwaondolea adha ya kutembea umbali mrefu kwa ajili ya kufuata huduma za afya.

Furaha hiyo imewapelekea Wananchi hao kutangaza shukrani zao kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kitendo cha kuelekeza fedha nyingi za miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Zahanati hiyo ambayo itaweza kuhudumia zaidi ya watu 2000 wakazi wa Kijiji hicho.

Bila kupepese macho wananchi hao wamesema wanaendelea kumuombea kwa Mwenyezi Mungu Rais Dkt. Samia ili aendelee kuwa na afya njema na azidi kutafuta fedha kwa kujenga na kuhimalisha miradi ya maendeleo na kusisitiza kwamba amekuwa mkombozi mkubwa cha changamoto ambazo wanawake walikuwa wakizipitia.

Wakizungumza na Waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuzinduliwa Zahanati hiyo wananchi wa Kijiji hicho wamesema kuwa kitendo cha kukosa huduma ya afya kwa ukaribu kulisababisha adha kubwa na wakati mwingine kupelekea baadhi ya akina mama kujifungulia njiani.

Hawa Mussa ni moja wa Wakunga ngazi ya Kata amesema Kijiji hicho ambacho kipo mpakani na Mkoa wa Manyara hakikuwa na huduma muhimu ya Zahanati jambo ambalo lilikuwa likisababisha usumbufu mkubwa hususani kwa akina mama waliokuwa wakihitaji huduma ya kujifungua sambamba na huduma za Watoto.

Amesema Kijiji hicho ambacho kina makabila mbalimbali wakiwepo Wamang'ati, Wanyaturu na Wabarabaigi kilikuwa na shida kubwa ya huduma hiyo ambapo kwa sasa huduma za afya kwa wananchi hao zinaenda kuimarika.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba amesema, Wananchi wote wa Kijiji hicho na waliopo jirani watanufaika na Zahanati hiyo na hayo ndiyo malengo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuona Watanzania wote afya zao zinaimarika.

Hata hivyo amewaomba Wataalamu wa huduma za afya katika Zahanati hiyo kuhakikisha wanakuwa karibu na wateja wao ambao ni wagonjwa na kutenga muda wa kutosha kuzungumza nao pindi wanapokuja kupatiwa huduma ili kubaini matatizo yao kabla ya kuwapatia matibabu.

“Wagonjwa wanatakiwa kupatiwa muda wa kuzungumza nao badala ya kutumia lugha kali na za vitisho hata wakati mwingine kuwapatia majibu ambayo pengine si ugonjwa husika”. Serukamba

Serukamba amewasihi Wauguzi kutambua kuwa huduma wanayoitoa inatakiwa kutolewa kwa watu wote bila ubaguzi hususani akina mama wajawazito pamoja na lugha rafiki hasa wakati wa huduma bila kujali anayehudumiwa anaishi mazingira mazuri au si mazuri.

Pamoja na hayo Serukamba ameuagiza uongozi wa Kijiji hicho kuhakikisha wanatunza mazingira kwa kupanda miti ya kutosha kwa lengo la kuifanya Zahanati kuwa katika mazingira mazuri safi na yenye kuvuti ili hata mama mjamzito anaposindikizwa pawe na mazingira rafiki kwa wasindikizaji kupumzika.

MATUKIO KATIKA PICHA WAKATI WA UZINDUZI HUO.




Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskas Muragili akizungumza na Wananchi kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Singida.







No comments:

Post a Comment