Wednesday, October 25, 2023

RC SERUKAMBA ATANGAZA MSAKO WA KUKAGUA MIRADI BILA KUPANGIWA

MKUU wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba ametangaza rasmi msako wa kutembelea miradi yote ya  maendeleo inayotekelezwa na Serikali katika Mkoa huo kwa lengo la kujiridhisha na utekelezaji wa miradi hiyo bila kuchaguliwa mradi wa kukagua.

Mkuu huyo wa Mkoa wa Singida amesema hayo jana tarehe 25 Oktoba, 2023 mara baada kuhitimisha ziara yake ya ukaguzi wa miradi katika Wilaya ya Singida, hatua hiyo ya kutembelea mradi mmoja baada ya mwingine kila Wilaya ni kutaka kuhakikisha utekelezaji wa miradi hiyo unafanyika kwa kiwango kinachotakiwa pamoja na ubora kwa thamani ya fedha iliyotolewa katika mradi husika ili wananchi wapate huduma bora na ya kiwango kinachostahili.

Akizungumza na Watendaji wa Mkoa huo Serukamba amesema Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuwa ikitoa fedha nyingi na kwa wakati kwa ajili ya maendeleo hivyo ni lazima ikatekelezwa kwa muda uliokusudiwa kwa manufaa ya Watanzania.

"Nitangaze kuwa baada ya wiki moja nitaanza ziara ya kutembelea mradi mmoja baada ya mwingine na sitahitaji kupangiwa ni mradi gani wa kutembelea nitahakikisha nafika kwenye kila mradi ambao unatekelezwa na nitatembelea miradi yote katika Halmashauri zote za Mkoa wa Singida”

"Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri zote za Mkoa huu na Waandisi hakikisheni mnajipanga vyema ni lazima miradi yote itekelezwe kwa wakati na nyie Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na Waandisisi nawaeleza msipende kukaa maofisini na kusubiria taarifa fikeni kwenye maeneo ya kazi kwa lengo la kuona kazi zinaendeleaje”

"Na wakati mwingine siyo kufika tu na kukagua kagua na mpango kazi wa Mkandarasi anayefanya kazi na ikitokea ukarudi ukakuta hajatekeleza makubaliano unaweza kubadilisha Mkandarasi mwingine na mafundi wengine lengo kubwa ni kazi kufanyika kwa kiwango na kwa ubora unaohitajika ili ikamilike kwa wakati" ameeleza Serukamba.

Hata hivyo Mkuu huyo wa Singida ameeleza kuwa kwa hatua ya sasa miradi ya afya inaendelea vizuri na inaridhisha lakini miradi ya elimu inatakiwa kuharakishwa zaidi na ifikapo mwezi Desemba mwaka huu iwe imekamilika kwa lengo la wanafunzi watakaoingia shule ya awali na kidato cha kwanza wawe na uhakika wa miundombinu yote ya shule.

Singida ni kati ya Mkoa ambao umepokea fedha nyingi za miradi ya maendeleo na ni miongoni mwa Mikoa ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amefurahishwa na utekelezaji wa miradi hiyo.






No comments:

Post a Comment