Sunday, October 01, 2023

SINGIDA YAADHIMISHA SIKU YA WAZEE DUNIANI, WAZEE 100 WAPATIWA BIMA YA AFYA

Mkoa wa Singida leo tarehe 1 Oktoba, 2023 umeadhimisha Siku ya Wazee Duniani kwa kuwapatia Bima ya Afya ya Jamii iliyoboreshwa (iCHF) Wazee miamoja (100) wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo na kuhusisha wawakilishi kutoka Halmashauri zote saba za Mkoa huo.  

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Singida katika Siku ya Wazee Duniani Jimson Mhagama ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni amesema suala la Wazee kupatiwa vitambulisho vya matibabu ni agizo la Serikali ili kuhakikisha wanatambuliwa na kupewa  huduma stahiki.

Mhagama amepongeza hatua nzuri iliyofikiwa katika uundwaji wa mabaraza ya wazee ambapo mabaraza ya Wazee 637 kati ya hayo mabaraza 151 sawa na asilimia 24 yamejengewa uwezo katika Mkoa wa Singida ili kuhakikisha huduma na maslai ya Wazee yanapatikana.

“Niwapongeze sana wadau wetu wa maendeleo kwa kazi kubwa mliofanya ya kuhakikisha wazee wanajengewa uwezo wa Sera ya wazee ya mwaka 2003 pamoja na majukumu ya viongozi wa mabaraza ya Wazee katika ngazi mbalimbali”

“Nawaelekeza Wakurugenzi wote wa Halmashauri kuhakikisha mabaraza ya Wazee yanafanya vikao vyao kila robo kama miongozo inavyoelekeza ili kuwezesha ufanisi katika kazi zake”. Amesema Mhagama kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba.

Aidha Serukamba ametoa rai kwa Jamii hasa ndugu wa karibu kuacha tabia ya kuwanyang’anya Wazee maeneo yao (ardhi, nyumba nk) jambo linalopelekea Wazee kukosa mwelekeo. Hivyo amesisitiza kuwa kitendo hicho ni kinyume na Sheria, na wale watakaobainiki Sheria itachukua mkondo wake.

Akizungumzia suala la malezi ya watoto, Mhagama kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo amesisitiza umuhimu wa wazazi kuwalea watoto wao ili kuwajengea stadi mbalimbali za maisha na kufanya wawe raia bora.

Kwa upande wa wazee wanaonufaika na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF Serikali Mkoani Singida imesajili kaya zipatazo elfu 58,760 zinazonufaika wakiwemo wazee, kati ya kaya hizo watoto ni elfu 1,318 kutoka kaya maskini ni wanufaika wa mfuko huo.

Hata hivyo Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba kupitia kwa mwakilishi wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni ametoa wito kwa vijana kuwatunza wazee wao ambao ni hazina kwa kuwatimizia mahitaji yao mbalimbali ikiwemo chakula ili kuepuka Wazee kuzunguka mitaani wakiombaomba.

Akimalizia hotuba yake Mkuu wa Mkoa wa Singida iliyosomwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni amewakumbusha na kuwaomba wazee kuendelea kusisitiza suala la malezi chanya kwa watoto na maadili mema kwa vijana ili kujenga jamii isiyokuwa na mmomonyoka wa maadili.

Mkoa wa Singida unandelea kuboresha huduma za Afya kwa Wazee, huduma za matunzo kwa Wazee wasio kuwa na uwezo kwa kuwatengea makazi yaliyopo Sukamahela katika Wilaya ya Manyoni Mkoani humo.

Kauli mbiu ya mwaka huu (2023) ambayo ni “Uthabiti wa Wazee kwenye dunia yenye Mabadiliko.

“Kauli mbiu hiyo inamaanisha kuwa Dunia inapitia mabadiliko mbalimbali ya kiuchumi, kijamii, kiutamaduni, kisiasa na dhihiri kuwa Wazee wamekuwa imara kwenye kukabiliana na mabadiliko hayo”.

No comments:

Post a Comment