Tuesday, October 17, 2023

RAIS DKT. SAMIA AHITIMISHA ZIARA YAKE MKOANI SINGIDA KWA KISHINDO, WANANCHI WAMSHUKURU KWA MIRADI YA MAENDELEO

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa fedha za miradi ya maendeleo mkoani humo na ameahidi ataendelea kusimamia miradi, sambamba na ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri saba za Mkoa huo kwa nia ya kutekeleza maono ya Rais ya utekelezaji miradi ya maendeleo kwa wananchi.

Serukamba akizungumza leo (tarehe 17 Oktoba, 2023) Wilayani Iramba wakati wa salamu kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ikiwa ni siku ya mwisho ya ziara yake ya kikazi aliyoifanya kwa siku tatu Mkoani humo kwa ajili ya kukagua miradi, kuizindua na kuweka jiwe la msingi kwenye miradi ya maendeleo.

Aidha, Serukamba amemuhakikishia Rais Dkt. Samia, kwamba kutokana na mambo mazuri yaliyofanywa kwa kipindi cha miaka miwili hususan katika sekta ya afya, kilimo, maji, nishati na nyingine ni hakika wanasingida watalipa deni hilo kwa kuhakikisha wanamchagua kwa kishindo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Mkuu wa Mkoa huyo amesema kuwa tangu Tanganyika ipate uhuru Rais Dkt. Samia amefanya maendeleo makubwa kwa wananchi nchi nzima hususan katika Mkoa wa Singida.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan (kulia) akiteta jambo kwa furaha na Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba (kushoto). Katikati ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati wa hitimisho la ziara ya Rais aliyoifanya Mkoani Singida kuanzia tarehe 15 Oktoba hadi 17 Oktoba Mwaka huu.

Akizungumzia Wilaya ya Iramba amesema kuwa Iramba ina vijiji 70 lakini kila kijiji kina mradi mkubwa wa maendeleo jambo ambalo Rais amafanya mambo yake kwa vitendo kwa manufaa ya wananchi wake.

Akizungumza kwenye hitimisho ya ziara hiyo, Serukamba amesema wananchi sio kwamba wanampenda Rais Dkt. Samia kwa kuwa anatoka katika Chama Cha Mapinduzi bali anapendwa kutokana na utendaji wake bora wa kazi ambao unaonekana na wenye kugusa maisha ya watu.

Amesema kutokana na hali hiyo wananchi wa Singida wana deni kwa Rais Samia na deni hilo litalipwa kwa awamu mbili ambapo ni katika uchaguzi wa Serikali za mitaa 2024 na deni lingine litalipwa kwa fidia mwaka 2025 kwa kuongoza kupiga kura nyingi kwa Rais, Mbunge na Diwani wanaotoka katika Chama Cha Mapinduzi.

Mwisho.


No comments:

Post a Comment