Tuesday, August 15, 2023

RC SERUKAMBA AZINDUA JENGO LA UTAWALA HALMASHAURI YA SINGIDA DC

MKUU wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, amezindua jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Singida na kuwataka Watumishi wa Halmashauri hiyo kulitunza jengo hilo na kutoa huduma bora kwa Wananchi bila kufanya upendeleo.

Akizungumza na Wananchi na Watumishi leo (Agosti 15, 2023) baada ya kuzindua jengo hilo, alisema  amewataka watumishi wahakikishe wanatoa huduma nzuri kwa wananchi na kutoshiriki vitendo vya kuomba rushwa kutoka kwa watu wanao wahudumia.

Serukamba aliwataka pia Watumishi na Madiwani kila mmoja apewe mti wa kupanda kuzunguka jengo hilo na kuhakikisha anautunza hadi unakuwa ili kutunza mazingira kuzunguka jengo hilo.

"Tutoe huduma nzuri kwa wananchi tusiombe rushwa, pia msitoe huduma kwa upendeleo itakuwa haina maana Serikali imetoa Shilingi bilioni 2.7 kwa ajili ya kujenga jengo hilo halafu huduma zianze kutolewa mbaya.

Aidha, Mkuu wa Mkoa aliwapongeza wananchi waliotoa eneo la kujenga jengo hilo la Halmashauri ambalo litasaidia kutoa huduma kwa wananchi.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Ester Chaula, alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2020/2021 ilitenga bajeti kwa ajili ya kuanza ujenzi wa jengo la utawala ambapo eneo la ujenzi lilipatikana katika kijiji cha Mwahango kata ya Ilongero.

Alisema Halmashauri imekwisha pokea Sh.bilioni 2.7 kutoka Serikali kuu kuanzia mwaka wa fedha wa 2020/2021 hadi 2022/2023 ambapo kiasi kilichotumika hadi sasa ni Sh.bilioni 2.6 ambazo zimetumika kununulia vifaa vya ujenzi, samani za ofisi pamoja na malipo ya mafundi.

Chaula alisema katika mwaka huu wa fedha wa 2023/2024 Halmashauri imetenga Sh.milioni 800 kwa ajili ya kuongezea samani za ofisi, kununua vifaa vya TEHAMA, kukamilisha uzio, eneo la kuegesha magari na uchimbaji wa kisima cha maji baada ya mahitaji kuongezeka.

Alisema wakati wa utekelezaji wa mradi huo, zilijitokeza changamoto zilizosababisha jengo la utawala kuchelewa kukamilika ambazo ni kuaribika kwa saruji wakati wa ujenzi wa miradi ya COVID 9, kupanda kwa bei ya vifaa vya ujenzi na kukosekana kwa maji.


Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini, Mheshimiwa Ramadhan Ighondo akizungumza wakati wa hafla hiyo.




MWISHO

No comments:

Post a Comment