Monday, June 05, 2023

"Tunzeni miundombinu ya maji na mlipe bili" RC Serukamba.

Wananchi Wilayani Ikungi Mkoani Singida wametakiwa kulinda na kusimamia miundombinu ya maji na kulipa bili kwa wakati ili kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji na kuondoa changamoto zilizokuwa zikiwakabili wakazi wa eneo hilo.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba alipotembelea miradi mbalimbali ya maendeleo iliyopo Wilayani hapo ikiwemo miradi ya maji Kituo cha Afya, Shule na Mabweni.

RC Serukamba amesema ni jukumu la kila mtu kuilinda miundombinu hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kuwasaidia wananchi kama ilivyotarajiwa.

Hata hivyo amewaagiza Viongozi Wilayani hapo kuhakikisha kunapandwa miti kwenye vyanzo vya maji na huku akizitaka kamati za watumia maji kuhakikisha wanakusanya fedha zitakazoweza kusaidia kurebisha miundombinu pindi itakapo haribika.

Kwa upande wake Meneja RUWASA wilaya ya Ikungi Mhandisi Hopeness Liundi amesema Mradi huo uliopo Kijiji cha Iglansoni unahudumia watu wapatao 8619 ambao utasaidia kupunguza muda mrefu uliyokuwa ukitumika na wananchi hao kufuata maji.

Liundi ameeleza kwamba Mradi huo utasaidia kupunguza migogoro kwenye familia iliyokuwa inasababishwa na ukosefu wa maji na kupunguza magonjwa ya kuambukiza yanayosababishwa na matumizi ya maji yasiyokuwa salama katika jamii.

Hata hivyo Meneja huyo ameeleza kwamba Mradi umechangia ongezeko la upatikanaji wa maji Wilayani hapo  kwa asilimia 1.2 kutoka asilimia 60.8 ya awali hadi kufikia asilimia  68 ya sasa.

MATUKIO MBALIMBALI KATIKA PICHA WAKATI WA ZIARA HIYO













No comments:

Post a Comment