Thursday, May 11, 2023

Wananchi Mkoani Singida watakiwa kupewa elimu ya kujizuia na ulemavu wa macho.

Wataalamu wa afya wametakiwa kutoa elimu kwenye mashule na jamii kwa ujumla  juu ya ulaji  wa lishe bora itakayosaidia kuondoa changamoto ya uono hafifu kwa jamii kwa kuwa imekuwa ni changamoto kubwa kwa Mkoa wa Singida.

Hayo yamesemwa na Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Fatma Mganga wakati akifunga kikao cha tathimini ya utekelezaji wa mradi wa mtoto angaza ulioko chini ya Shirika la Sightsavers  kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hotel ya Regency  iliyopo Manispaa ya  Singida.

Aidha ameagiza Maafisa Lishe na Maafisa kilimo Mkoani hapo kutoa elimu na kusaidia wananchi kwenye kilimo cha bustani za mazao ambayo virutubishi vyake vitasaidia kuongeza ulinzi wa macho ili yasiweze kupoteza uono wake.

Hata hivyo RAS ameagiza kusambaza Mkoa mzima taarifa za uwepo wa huduma ya matibabu kwa gharama nafuu yanayoendelea katika hospitali ya rufaa Mandewa zifikishwe kwa jamii husika kwa kuwa wengi wanachangamoto hizo lakini hawajui wapi pa kupata msaada.

Amesema uono hafifu unaweza kuchangia kushuka kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa  ujumla  na kushuka viwango vya elimu endapo walimu hawataweza kuwapanga watoto darasani kulingana na  uwezo wa macho yao hivyo kutoa  maelekezo kwa walimu kuhakisha kunakuwa na mpangilio wa uukaaji darasani.

Kwa upande wake Meneja miradi ya Sightsavers, Edwini Maleko amesema Mkoa wa Singida umeweza kufaidika na miradi ya Sightsavers kwa kuwa zaidi ya Tsh. Bilioni 7 zimetumika katika maeneo mbalimbali Mkoani hapo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa nyumba, vifaa tiba na kusomesha Watumishi wa Afya katika hospitali ya Muhimbili na Nchini India.

Maleko amesema tatizo la uoni hafifu mkoani Singida ni kubwa ambapo asilimia 2.8 wana ulemavu wa macho na wanatakiwa kupata matibabu ili kuondokana na kadhia hiyo.

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Ernest Mugeta akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Dkt. Fatma Mganga ili kufunga kikao cha tathimini ya utekelezaji wa mradi wa mtoto angaza.

Meneja miradi ya Sightsavers, Edwini Maleko akizungumza wakati wa kikao cha tathimini ya utekelezaji wa mradi wa mtoto angaza.



No comments:

Post a Comment