Wednesday, May 10, 2023

TAKUKURU kuchunguza tozo za soko la Vitunguu Singida

MKUU wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba ameiagiza Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU mkoani hapo kuchunguza uhalali wa fedha wanazotozwa wafanya biashara wa Soko la vitunguu Misuna lililopo kata ya Misuna  katika Manispaa ya Singida na kuwachukulia hatua wote watakao bainika kuchukua fedha kinyume na utaratibu.

Serukamba ameyasema hayo alipotembelea soko hilo na kusikiliza kero za wafanya biashara ambapo wengi walilalamikia kutozwa sh.200 kwa kila gunia la vitunguu, kila wiki washusha mizigo hutoa 5000, kila gari likiangia linachajiwa 10,000 na madalali kutoa 2,000 fedha zote hizo hakuna risiti inayotolewa huku wakiendelea kutoa ushuru wa soko hilo.

Amesema utaratibu ni kwamba kila fedha inayotolewa lazima mtoaji apewe risiti vinginevyo zinapotelea kwenye mifuko ya watu hivyo kuwaagiza TAKUKURU kuchunguza kama kuna jinai wawachukulie hatua huku akiitaka taasisi hiyo kujikita zaidi kwenye kuzuia zaidi ili hali hiyo isiendelee.

Malalamiko mengine ni ukosefu wa miundombinu ya soko kama uzio, uchafu kutozolewa kwa wakati hivyo kusababisha harufu kali na kukosekana  kivuli au vizuizi vya mvua au jua jambo ambolo RC Serukamba alimuagiza Mkurugenzi wa Manispaa kuanza kufunika eneo hilo kwa awamu na kazi hiyo ianze kabla ya mwezi wa Saba.

Hata hivyo  Mkuu wa Mkoa huyo amepiga marufuku wafanya biashara kutozwa ushuru mara mbili ndani ya Mkoa mmoja na kuwataka Wakuu  wa Wilaya kulisimamia kwa kuwa watakaoumia  ni wakulima.

Marufuku hiyo imetokana na malalamiko ya wafanya biashara kulalamikia mageti ya Manyoni na  Kintinku ambapo wamesema wanapoteza muda mrefu kwa ukaguzi ambao unafanyika sokoni na vibali wamepewa.

Aidha Serukamba amesema atawasiliana na Mamlaka husika ili kuhakikisha nchi nzima wanakuwa na kipimo cha gunia la vitunguu unaofanana ili kuleta ushindani sawa.

"Haiwezekani Singida tunajaza gunia kwa vipimo vya Serikali ambapo tunapinga rumbesa lakini maeneo mengine wanaachwa hii haileti ushindani sokoni' Alisema Serukamba.

RC Serukamba ametoa wito kwa wafanyabiashara kufuata sheria kanuni na taratibu katika biashara zao ili kuondoa changamoto ambazo zinawakabili maeneo mbalimbali.

MATUKIO MBALIMBALI KATIKA PICHA

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba akizungumza na wafanyabiashara katika soko la vitungu.




Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhadisi Paskas Muragili akizungumza wakati wa ziara hiyo.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Singida Mheshimiwa Yagi Kiaratu akizungumza wakati wa ziara hiyo.

Mwenyekiti wa Soko la Vitunguu mkoani Singida Iddy Mwanja akizungumza wakati wakati  Mkuu wa Mkoa wa Singida alipotembelea soko.



No comments:

Post a Comment