Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi Celina O. Kombani akiwa katika moja ya chumba cha upasuaji katika Hospitali Mpya ya Rufaa ya Mkoa wa Singida, Pembeni yake ni Mkuu wa Wilaya ya Singida Said Amanzi na mwenyeji wake Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Parseko Kone.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi Celina O. Kombani ameahidi kuhakikisha kuwa madaktari wanapatika ili huduma za rufaa zianze kupatikana katika hospitali Mpya ya rufaa ya Mkoa wa Singida.
Waziri Kombani ametoa ahadi hiyo leo asubuhi alipotembelea Hospitali hiyo kuona hali halisi na kupokea taarifa ya mahitaji ya madaktari na watumishi wengine ili huduma za rufaa zianze kutolewa.
Amesema hospitali hiyo ina majengo mazuri ambapo fedha za serikali zimetumika katika kuijenga hivyo kinachotakiwa ni kupatikana kwa watumishi hao ili wananchi wanufaike na hospitali hiyo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi Celina O. Kombani akitoka nje ya Hospitali Mpya ya Rufaa ya Mkoa wa Singida, Kushoto kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Parseko Kone na kulia kwake ni Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa Aziza Mumba.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Parseko V. Kone amemkabidhi Waziri Kombani maombi ya kupatiwa watumishi wa kada ya afya 166 kwa ajili ya hospitali mpya ya rufaa.
Dokta Kone amesema tangu mwaka 2013 majengo ya wagonjwa wa nje (OPD), jengo la wazazi, jengo la uchunguzi wa magonjwa na jengo la kuhifadhia dawa za chanjo yalikamilika na hivyo hospitali hiyo inahitaji madaktari bingwa watano ili huduma za rufaa zianze kutolewa kwa akina mama.
Ameongeza kuwa watumishi wanaohitajika ni pamoja na madaktari, madaktari wasaidizi, wauguzi, wahudumu wa afya, wateknolojia wa maabara, wateknolojia wa mionzi, maafisa lishe na afya.
Hospitali mpya ya rufaa ya Mkoa wa Singida ilianza kujengwa mwaka 2009 na makisio ya garama za ujenzi wa hospitali hiyo hadi itakapokamilika ni shilingi bilioni 350. Hospitali hiyo itahudumia mikoa jirani 6 inayozunguka Mkoa wa Singida na itakuwa hospitali pekee ya rufaa ya serikali katikati ya nchi.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dokta Parseko Kone akizungumza na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi Celina O. Kombani nje
ya Hospitali Mpya ya Rufaa ya Mkoa wa Singida, kulia ni Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa Aziza Mumba.
Sehemu ya mbele ya jengo la wagonjwa wa nje (OPD) katika Hospitali Mpya ya Rufaa ya Mkoa wa Singida.
No comments:
Post a Comment