Friday, April 28, 2023

Lugha zisizo na staha za Watendaji zamkera Serukamba

Watendaji wa Serikali Mkoani Singida wametakiwa kujifunza na kutumia taaluma ya huduma kwa mteja (costumer care) ili kutoa huduma inayowaridhisha wateja wao na kupunguza kero kwa wananchi.

Kauli hiyo imetolewa leo 28/4/2023 na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba wakati alipokuwa akisikiliza kero za Wananchi wa Manispaa ya Singida katika Mkutano uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA).

Amesema changamoto nyingi zinasababishwa na lugha mbaya za Watendaji wa Serikali ambao wameamua kutojali maslahi ya wengine hivyo kuwataka kutumia lugha zenye staha kuwajibu wateja wao na kujiwekea taratibu za kuwapa elimu kabla ya kufanya maamuzi.

Aidha amewataka Wakuu wa Taasisi mkoani hapo kuhakikisha wanatekeleza maamuzi wanayokubaliana vinginevyo vikao hivyo vitakuwa havileti maana kwa wananchi ambapo waliokuwepo baadhi ya wananchi ambao walikuja na hoja ambazo zilitolewa maelekezo katika kikao kilichopita.

Kero nyingi zilizoletwa na wananchi kwa Mkuu wa Mkoa zilikuwa ni migogoro ya viwanja, changamoto ya ulipaji wa pensheni kwa wastaafu kupitia mfuko wa NSSF, migogoro ya familia na  umilikishwaji wa ardhi.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt. Fatma Mganga, Mkuu wa Wilaya ya Singida Muhandisi Paskas Muragili, Mstahiki Meya, Wahandisi, Kamati ya ulinzi na usalama na maafisa elimu kata pamoja na wakuu wa Taasisi.

MATUKIO KATIKA PICHA

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba akizungumza wakati wa mkutano huo.

Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Fatma Mganga akizungumza wakati wa mkutano huo.

Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskas Muragili akizungumza wakati wa mkutano huo.

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida akijibu moja ya kero za wananchi wa Singida Mjini.















Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba akisisitiza jambo kwa Meneja wa NSSF Mkoa wa Singida mara baada ya mkutano huo.

No comments:

Post a Comment