Monday, August 22, 2022

Pikipiki Tisa zenye thamani ya shilingi Milioni 29.2 zakabidhiwa kwa watendaji wa RUWASA Singida.


Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba leo tarehe 22.08.2022 amekabidhi pikipiki 9 zenye thamani ya shilingi  Milioni 29.2 kwa watendaji wa Wakala wa Maji Safi na usafi wa mazingira  vijijini RUWASA  ngazi za wilaya na Jumuiya za watumia maji ili kurahisisha usimamizi na uendeshaji wa miradi ya Vijijini.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba  akiongea na wafanyakazi wa RUWASA katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Bonde la Kati mkoa wa Singida.

Akiongea na wafanyakazi wa RUWASA katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Bonde la Kati RC Serukamba amewataka watendaji hao kuhakikisha pikipiki hizo zinatunzwa ili ziweze kutumika kwa muda mrefu na kuhakikisha zinafanyiwa matengenezo kwa wakati.

Aidha amewataka wote waliyopata vitendea kazi hivyo kuhakikisha zinatumika kwa shughuli za usimamizi wa Miradi ya maji na kuwataka kwenda kutatua kero za Wananchi ikiwa ni pamoja na kusaidia urekebishaji wa miundombinu ya maji.

Hata hivyo RC Serukamba amewataka Mameneja hao kuhakikisha kwamba wanatekeleza maagizo ya Waziri wa Maji  ya kuhakikisha maji yatauzwa kuanzia sh. 50 kushuka chini kwa uzalishaji wa maji kwa kutumia dizeli, uzalishaji wa maji kwa kutumia umeme sh. 40 na uzalishaji wa maji kwa kutumia sola sh. 30 kwa ndoo.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba  akiongea na wafanyakazi wa RUWASA katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Bonde la Kati mkoa wa Singida.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa Singida Alhaji Juma Kilimba ameeleza kwamba uboreshaji na  usambazaji wa maji vijiji ni moja ya agenda ya Ilani ya chama hicho ambapo amewataka kuhakikisha zinatumika kulingana na malengo yaliyopangwa.

Amesema nitegemeo la chama kwamba ugawaji huo wa vyombo vya usafiri utakuwa ni endelevu hasa katika jumuiya  za watumiaji maji ambapo huko ndipo wananchi wanakopata changamoto.

Awali akisoma taarifa yake Meneja Ruwasa Mkoa wa Singida Mhandisi Lucas Said amesema pikipiki hizo zimegawanywa katika Wilaya ya Ikungi, Manyoni, Itigi, Iramba, Mkalama na Mamlaka ya maji Kiomboi.

Aidha amesema katika mwaka wa fedha wa 2021/22 Serikali iliwatengea Bilioni 14.9 ambapo kufikia June wameshapata fedha hizo kwa asilimia 92.

Mhandisi Lucus amesema upatikanaji wa maji safi katika maeneo ya mjini ni asilimia zaidi ya 62 huku akibainisha kwamba eneo la manyoni hali ya upatikanaji wa maji sio mzuri na jitihada zinaendelea kuboresha mazingira hayo.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba  (wapili kutoka kushoto) na Mwenyekiti wa CCM mkoa huo wakiwa kwenye pikipiki kama ishara ya uzinduzi rasmi wa zoezi la ugawaji kwa Watendaji wa RUWASA ngazi ya wilaya na Jumuiya ya watumiaji wa maji wakati wa hafla ya makabidhiano yaliyofanyika katika ofisi za Bonde la Kati mkoani humo.

Meneja Ruwasa Mkoa wa Singida Mhandisi Lucas Said akisoma taarifa ya ugawaji wa pikipiki kwa Watendaji wa RUWASA ngazi ya wilaya na Jumuiya ya watumiaji maji.

Wafanyakazi wa RUWASA ngazi ya wilaya na Jumuiya ya watumiaji maji wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya pikipiki iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Bonde la Kati mkoa wa Singida.

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Singida (kulia) akizungumza jambo na Mkuu wa Mkoa huo Mheshimiwa Peter Serukamba mara baada ya hafla ya makabidhiano ya pikipiki. (kulia) ni Meneja wa RUWASA mkoa wa Singida Mhandisi Lucas Said.

No comments:

Post a Comment