Thursday, December 01, 2022

Halmashauri za Mkoa wa Singida zashauriwa kujenga magorofa, zapongezwa kwa usimamizi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa.

 

Halmashauri za Wilaya Mkoani Singida zimeshauriwa kubadilika na kuanza kufikiria kujenga shule za ghorofa ili kuokoa maeneo ya ardhi ambayo yangeweza kutumika  kwa shughuli nyingine za maendeleo.

Ushauri huo umetolewa  leo na Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba, alipokuwa akiendelea na ziara yake ya ukaguzi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Wilaya ya Singida Vijijini, Ikungi na Manispaa.

Amesema kwa kuwa miji inapanuka kwa kasi na ardhi inakuwa ndogo hivyo ni muhimu kuanza kujenga majengo kwa  kwenda juu ili kupunguza matumizi ya ardhi.

Aidha amezipongeza Halmashauri za Singida, Ikungi na Manispaa kwa kazi nzuri ya usimamizi wa vyumba vya madarasa ambayo imefikia asilimia zaidi ya 80.

Awali akiwa katika Wilaya ya Singida amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kutumia fedha za ndani kuongeza baadhi ya vyumba vya madarasa badala ya kusubiri zinazotolewa na Serikali.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Singida DC Ester Chaula,  amesema Halmashauri ya Wilaya hiyo ilipokea jumla ya  Tsh. Bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 50 katika shule 17 za Sekondari.

Aidha Mkurugenzi ameeleza kwamba baada ya fedha hizo ziliwekwa katika akaunti 17 za shule hizo ambapo ameeleza kwamba kwa sasa shule hizo zipo katika hatua ya umaliziaji.

Jumla ya shilingi Milioni 581.49 zimeshatumika katika utekelezaji wa ujenzi wa madarasa hayo ambayo kwasasa madarasa hayo yamefikia asilimia 85 na wameahidi kukamilisha mpaka uwekaji wa madawati kabla ya tarehe 15 Desemba, 2022.

Aidha kwa upande wake Meya wa Manispaa ya Singida Yagi Kiaratu, amesema Manispaa imepokea fedha kiasi cha Bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 50 vya madarasa ya wanafunzi wa kidato cha kwanza.

Ameendelea kusema kwamba vyumba 8 vipo katika hatua ya upakaji wa rangi, vyumba 26 vipo hatua ya skiming wakati vyumba 14 vikiwa katika hatua ya kupiga ripu na viwili (2) katika hatua ya upasuaji.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Ikungi Faraja Maluga, ameeleza kwamba Wilaya ya Ikungi imepatiwa jumla shilingi 580 Milioni kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 29 katika shule 16.

Mkurugenzi huyo ameeleza kwamba madarasa hayo yote yamefikia asilimia 80 na wanategemea kukabidhi kwa muda iliyopangwa.

Mkoa wa Singida umepewa fedha jumla ya Bilioni 5.8 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 290 kwa wanafunzi wa mwaka 2023 katika Halmashauri Saba (7) za Mkoa wa Singida.

MATUKIO MBALIMBALI KATIKA PICHA

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba (kulia) akipokea taarifa ya ujenzi wa vyumba vya madarasa mapema leo wakati wa ziara yake Singida Vijijini leo tarehe 1 Desemba, 2022. Kulia kwake ni Mkurugenzi wa Singida Vijijini Ester Chaula


Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba (kulia) akifafanuliwa jambo kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida Jeshi Lupembe wakati wa ziara ya ukaguzi wa majengo ya madarasa.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba akiagana na viongozi mbalimbali wa Chama Tawala na Serikali wakati alipomaliza ziara yake ya kukagua ujenzi wa vyumba vya madaraka katika Halmashauri ya Manispaa ya Singida 1 Desemba, 2022

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba (kushoto) akizungumza na kupongeza viongozi wa Wilaya ya Ikungi kwa usimamizi bora wa vyumba vya madarasa wakati wa ziara yake 1 Desemba, 2022

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro (kushoto) akimuelezea Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba kuhusu maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 







Mkuu wa Mkoa Peter Serukamba akipokea taarifa mbalimbali za hali ya ujenzi wa vyumba vya madarasa​

Ziara ya ukaguzi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa Wilayani Ikungi ikiendelea

No comments:

Post a Comment