Tuesday, November 29, 2022

Ushirika Imara ndio utakaobadilisha hali ya Kilimo Mkoani Singida - RC Serukamba

 

Viongozi wa vyama vya Ushirika wa Kilimo Mkoani Singida wametakiwa kuhakikisha wanasimamia Ushirika uimarike ili kuwasaidia wakulima kupata pembejeo za kilimo, utaalamu na masoko ya bidhaa zao.

Kauli hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba, alipokuwa anafungua Mkutano Mkuu wa 27 wa Ushirika kwa mwaka 2022 uliofanyika katika ukumbi wa Kanisa Katoliki (Social) uliopo Singida Mjini ambapo ameeleza umuhimu wa uwepo wa Ushirika imara ambao utasaidia kuondoa changamoto za wakulima.

Amesema vyama vya Ushirika kwa sasa havina msaada mkubwa kwa wakulima kwa kuwa haviwasaidii kupata pembejeo wala masoko na utaalamu ikilinganishwa na ushirika wa kipindi cha nyuma ambapo wanaushirika waliweza kusomesha watoto wao kwa kupitia ushirika huo.

"Lazima tutafute msingi wa Vyama vya ushirika ili viweze kuwasaidia na kuwakomboa wananchi kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma ambapo uliweza kusaidia kusomesha na ulisaidia kudai Uhuru" RC Serukamba

Aidha Serukamba amesisitiza uwepo wa uwazi katika shughuli za Ushirika kwa kuwa chombo hicho ni cha hiyari kujiunga hivyo ni muhimu kuwepo kwa uwazi ili wanachama wajue kinachoendelea katika  vyama vyao.

Hata hivyo Serukamba amefafanua kwamba wapo wakulima ambao walipeleka mazao yao katika ushirika lakini mpaka sasa hawajaweza kupata fedha zao kutokana na ushirika kushindwa kuwatafutia masoko ya uhakika.

RC ameelekeza wakulima kabla ya kutambua aina ya zao analolima ni muhimu kuanzia sokoni ili kujua mahitaji ya soko ambapo alisema kwamba ni jukumu la ushirika ulio imara.

Akimalizia hotuba yake amesema ushirika ndio chombo pekee ambacho kitaondoa utapeli na madalali katika Kilimo ambao husababisha wakulima kuuza mazao yao yakiwa shambani kwa bei ndogo.

Mkutano huo ulihudhuriwa na Viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskasi Muragili, Meya wa Manispaa ya Singida Yagi Kiaratu, Kamishina wa Tume ya Ushirika pamoja na Naibu Mrajisi wa Vyama vya ushirika.

No comments:

Post a Comment