Tuesday, November 08, 2022

RAS Singida atembelea Hospitali, vituo vya Afya

Katibu Tawala Mkoa wa Singida Mwl. Dorothy Mwaluko leo tarehe 8.11.2022 ametembelea Hospitali, vituo vya Afya na Zahanati vilivyopo Wilaya ya Singida vijijini na Mkalama ili kuona huduma za afya zinavyotolewa katika maeneo hayo.

 Akiwa katika ziara hiyo amekagua Watumishi na utendaji kazi wao vitendea kazi pamoja na usafi wa mazingira yanayozunguka maeneo hayo.

Dorothy akiwa katika Kituo cha Afya cha Kinyangiri kilichopo kata ya Kinyangiri Wilayani Mkalama  amewaagiza Waganga wafawidhi katika Hospitali, Zahanati na vituo vya Afya kusimamia huduma stahiki kwa wagonjwa, maadili ya kazi na utunzaji wa mazingira ya nje na ndani ya Hospitali ili kuboresha mandhari ya maeneo hayo.

Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dorothy Mwaluko (kulia) akisisitiza jambo kwa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida Daktari Victorina Ludovick wakati wa ziara hiyo.

"Nataka mpande miti katika maeneo yenu na pia nataka kuwe na utaratibu wa upangaji wa vitu Hospitalini (classification) kama ulivyo utaratibu" alisema Mwaluko

Katibu Tawala huyo akiwa Kinyangiri akamuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida Daktari Victorina Ludovick kuhakikisha gari la wagonjwa aina ya landrova linafanyiwa matengenezo haraka ili liweze kutumika kwa ufanisi mkubwa.

Hata hivyo Mwaluko akaagiza kuanza kutumika majengo yote ambayo fedha za umma zimetumika zikiwemo nyumba za wafanyakazi wa sekta ya Afya kuanza kutumika haraka iwezekavyo.

Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dorothy Mwaluko (kushoto) akisisitiza jambo kwa Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mkalama (kulia) pamoja na Mganga Mfawidhi Hospitali ya Wilaya ya Mkalama wakati wa ziara hiyo.

Aidha akawataka viongozi wa Idara ya Afya Mkoani hapo kutafuta miradi mbalimbali ambayo itawasaidia kuendesha shughuli mbalimbali badala ya kutegemea fedha za Serikali.

Aidha ameiagiza timu ya  usimamizi na uendeshaji wa huduma za Afya ya Mkoa huo  (RHMT) kuwatembelea watumishi wa Afya mara kwa mara ili kuwafariji na kuona na kutatua changamoto zinazowakabili.

Naye Mganga mfawidhi wa Kituo cha Kinyangiri Daktari Anna Kimonga akamueleza Katibu Tawala Mkoa kwamba  Kituo hicho kinapokea  Wagonjwa kati ya 30 mpaka 50 na wanawake wanaojifungua ni kati ya 25 mpaka 30 kwa mwezi ambapo ameeleza kwamba ni muhimu kuwa na gari la Wagonjwa lenye uwezo wa kufanya kazi kulingana na mazingira.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mkalama  Daktari  Dorisila John amesema  upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika Wilaya hiyo unaridhisha huku akibainisha kwamba kwa mujibu wa muongozo bado Kkna uhitaji wa madaktari na wauguzi katika vituo vingi vya Afya na Zahanati Wilayani hapo.

Dorisila amesema katika Hospitali ya Wilaya ya Mkalama mpaka kufikia tarehe 16 Novemba, 2022 ufungaji wa vifaa vya X-Ray utakuwa umekamilika jambo ambalo wanategemea kwamba huduma za mashine hiyo zitaanza hivi karibuni.

Ziara hiyo ya Katibu Tawala Mkoa wa Singida aliambatana na timu ya usimamizi na uendeshaji wa huduma za Afya Mkoa (RHMT) ambapo walitembelea Zahanati ya Kanisa Katoliki Iguguno, Kituo cha Afya Kinyangiri, Hospitali ya Wilaya ya Mkalama, Hospitali ya rufaa ya Iambi, Hospitali ya Wilaya ya Singida na Kituo cha afya Ilongero.

No comments:

Post a Comment