Thursday, September 08, 2022

“Ukusanyaji wa mapato kwa mkoa wa Singida ni swala la kufa na kupona” RC SERUKAMBA

 

Wakurugenzi wa Halmashauri Mkoani Singida wametakiwa kuunda Kamati ndogo ambazo zitakuwa zikikutana kwa wiki mara mbili katika kila Halmashauri ili kutathimini mapato ya kila chanzo cha fedha huku Madiwani waliotumia fedha za Halmashauri kinyume na utaratibu wakipewa siku tano kurejesha fedha hizo.

Akiongea katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba amesema ni lazima kuundwa kwa kamati hizo ambazo zitashughulikia upotevu wa mapato katika kila Halmashauri kwa kuwa swala hilo ni la kufa na kupona.

Aidha ameonya tabia ya baadhi ya Watendaji ambao wengi wao wanakusanya hela katika vyanzo mbalimbali vya fedha pasipo kuipeleka Benki jambo ambalo limekuwa likisababisha upotevu wa fedha za Halmashauri.

Hata hivyo ametumia Mkutano huo wa Baraza la Madiwani kuwaonya Madiwani wote ambao wanahusika na ukusanyaji wa mapato kazi ambayo ingefanywa na watendaji wa Halmashauri, huku akiwaasa Madiwani kutenganisha majukumu yao ili waweze kuwasimamia.

"Madiwani tuepuke kufanya vitendo ambavyo vitasabisha kushindwa kuwasimamia Watendaji, ukianza kukusanya Kodi ikatokea upotevu hakuna atakayeweza kukuuliza na Mtendaji akifanya kosa hilo hutaweza kumuwajibisha". Alisema Serukamba

Amesema kiwango cha makusanyo katika kipindi cha robo mwaka kwa baadhi ya Halmashauri Mkoani hakiridhishi hivyo ni jukumu la kila Mkurungezi wa Halmashauri kupitika upya vyanzo vyake vya mapato na kuhakikisha fedha hazipotei.

Hata hivyo RC Serukamba amewakumbusha Madiwani na Watendaji wa Kata na Vijiji kuhakikisha kwamba wakulima wanaanza kuandaa mashamba yao kwa wakati kwa kuwa Mkakati wa Mkoa kwa mwaka huu ni kuongeza uzalishaji wa mazao ya alizeti mahindi mpunga mbaazi na viazi.

Amesema Mkoa umejipanga kuongeza uzalishaji wa alizeti kwa kuongeza maeneo ya kulima ili kulifanya Taifa lijitosheleze kwa mafuta ya kula huku akifafanua kwamba Serikali imeboresha mazingira ya kilimo kwa kupunguza bei ya mbolea na ruzuku katika mbegu Bora za kilimo.

RC Serukamba amewataka Madiwani na Watendaji kuendelea kuwahamasisha wananchi kukata Bima ya afya ya CHF iliyoboreshwa ili kuimarisha Afya za watu na kuimarisha uchumi wao.

No comments:

Post a Comment