Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Singida,
Saidi Alli Amanzi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Singida, akifungua hafla ya
makabidhiano wa mradi wa afya ya mama na mtoto (SUSTAIN-MNCH). Wa kwanza kulia
ni Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Gishuli Charles na anayefuatia ni mwakilishi wa Mkurugenzi
wa shirika la World vision Tanzania, Mary Lema.
Shirika lisilo la kiserikali
World Vision Tanzania, limetumia zaidi ya shilingi 5.3 bilioni kugharamia mradi
wa kuboresha afya na lishe ya mama na mtoto Mkoani Singida.
Hayo yamesemwa na
Mwakilishi Mkurugenzi wa Miradi ya World Vision Tanzania Mary Lema, wakati akitoa taarifa yake kwenye
hafla ya makabidhiano ya mradi wa afya na lishe ya mama na mtoto
(Sustain-MNCH).
Amesema mradi huo umetekelezwa
katika wilaya za Iramba, Mkalama, Ikungi na Singida Vijijini na umedumu kwa
miaka mitatu kuanzia januari 2012 hadi mwezi Machi 2015.
Akifafanua, amesema mradi
ulijikita zaidi katika kuimarisha mfumo wa afya katika ngazi ya mbalimbali za
utoaji wa huduma za afya na lishe ya mama na watoto.
“Mradi umetoa mafunzo kwa
watendaji 325 na wasimamizi wa huduma za afya ya mama na mtoto ngazi mbalimbali
kwa lengo la kuwajengea uwezo juu ya upangaji na matumizi ya rasilimali
zilizopo. Pia mradi umeimarisha mafunzo ya utoaji taarifa za afya (MTUHA) kwa
wakati”,amesema Lema.
Baadhi ya wadau wa afya
waliohudhuria hafla ya makabidhiano ya mradi wa afya ya mama na mtoto (SUSTAIN
-MNCH) iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Aque Vitae Resort mjini
Singida.
Aidha Mwakilishi huyo amesema
malengo ya mradi huo yamefikiwa kwa kiwango kizuri ambapo idadi ya
wanawake wajawazito waliohudhuria kliniki mara 4 wakati wa ujauzito imeongezeka
kutoka asilimia 43 wakati mradi unaanza, hadi asilimia 50 wakati tathimini ya
mwisho inafanywa.
“Pia idadi ya akina mama wanaojifungulia
katika vituo vya kutolea huduma imeongezeka kutoka asilimia 62 wakati mradi
unaanza hadi asilimia 71 kwa sasa”,amesema.
Lema amesema shirika la World
Vision lilifikia uamuzi wa kutekeleza mradi huo Mkoani Singida ikiwa ni njia
moja wapo ya kuunga mkono juhudi za serikali kutekeleza mikakati mbalimbali ya
kuboresha afya na lishe ya mama na mtoto nchini iliyoridhiwa na umoja wa
mataifa.
Afisa afya Mkoa wa Singida,
Joseline Ishengoma, akiwasha gari aina ya Land cruiser lililotolewa msaada na
shirika la World vision Tanzania kwa hospitali ya mkoa mjini hapa.
Naye mgeni rasmi katika hafla
hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Parseko V. Kone ametumia fursa hiyo kuishukuru serikali ya
Canada kupitia shirika lake la maendeleo la Department of Foreign Affairs and
Trade Development (DFDAT) kwa kuufadhili mradi huo.
Katika hotuba yake iliyosomwa kwa
niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Singida Saidi Amanzi amesema, mradi huu
umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo vya akina mama na watoto katika
wilaya za Iramba, Mkalama, Singida Vijijini na Ikungi.
“Kwa kipindi cha mwaka 2011-2013,
vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi vilipungua kutoka vifo 52 hadi kufikia
vifo 49, na vifo vya watoto wachanga wenye umri kuanzia siku ya kuzaliwa hadi
siku ya 28, vimepungua kutoka 182 hadi 178”,amesema.
Dkt. Kone amesema mafanikio hayo
yametokana na kuimarika kwa mifumo ya utoaji wa huduma ambapo watoa huduma 101
walipata mafunzo ya utoaji huduma za dharura.
Twakwimu zinaonyesha kuwa Tanzania
ni miongoni mwa nchi 10 duniani zinazochangia katika asilimia 61 ya vifo vya
akina mama vitokanavyo na uzazi na asilimia 66 ya vifo vya watoto wachanga.
Kwa mujibu wa takwimu za Tanzania
Demographic and Health Survey (TDHS 2010), akina mama wapatao 454 hupoteza
maisha kati ya vizazi hai 100,000 ikionesha mafanikio kidogo ukilinganisha na
(TDHS 2004/2005 ya vifo 578 kwa kutoa kizazi hai 100,000.
Kasi hii ni ndogo sana
ukilinganisha na lengo la kitaifa la kufikia vifo 193 kwa kila vizazi hai
100,000 ifikapo desemba 2015.
Kwa upande wa vifo vya watoto
wachanga wenye umri wa kuanzia siku ya kuzaliwa hadi siku 28, wapatao 26 kati
ya vizazi hai 1,000 hupoteza maisha ambayo ni sawa na watoto 42,343 kwa mwaka.
Nusu ya vifo hivyo hutokea ndani ya saa 24 baada ya kuzaliwa.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Singida
ambaye n Mkuu wa Wilaya ya Singida, Saidi Alli Amanzi (wa tatu kulia) akiwa
pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya afya mkoani hapa waliohudhuria hafla ya
makabidhiano wa mradi wa afya na lishe kwa mama na watoto.
Na Nathaniel Limu, Singida
No comments:
Post a Comment